Mwalimu: Tutaibadili Uyole kuwa kitovu cha biashara Afrika

Mbeya. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ameahidi kuwa endapo atachaguliwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, serikali yake itaanzisha mpango kabambe wa kuliboresha eneo la Uyole, mkoani Mbeya.

Amesema ataboresha eneo hilo kwa kujenga kituo cha kimataifa kitakachokuwa mfano wa ukaribisho wa Tanzania kwa wageni kutoka nje na ndani ya nchi.

Mgombea huyo wa urais, amesema kituo hicho kitakuwa na huduma mbalimbali za kisasa zinazolenga kuwahudumia wasafiri, wafanyabiashara na wageni wanaoingia nchini kupitia ukanda wa kusini, kwa lengo la kuimarisha biashara za mipakani, kukuza utalii na kuongeza ajira kwa wananchi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.


Akihutubia mkutano wa kampeni mkoani Mbeya uliofanyika leo, Jumamosi Septemba 27, 2025, katika eneo la Uyole, Mwalimu amesisitiza kuwa eneo hilo lina fursa kubwa zisizotumika ipasavyo, licha ya kuwa na umuhimu wa kipekee kijiografia na kiuchumi.

Ameeleza kuwa Uyole ni lango kuu linalounganisha Tanzania na mataifa jirani yasiyo na bandari kama DRC Congo, Zambia, Malawi, Lesotho na Afrika Kusini, hivyo lina nafasi kubwa ya kuchochea maendeleo ya kikanda endapo litawekewa miundombinu ya kisasa na kuwezeshwa kuwa kituo cha kimkakati kwa biashara na usafirishaji.

 “Ilivyo hivi haifai. Tukichukua nchi, tutaitengeneza Uyole hadi hamtaamini. Nchi hii kufanya mambo makubwa inawezekana. Tofauti yetu na wengine ni kasi ya utekelezaji,” amesema Mwalimu huku akisisitiza kuwa serikali yake haitavumilia uzembe au uswahiba kazini.

Katika kuonyesha msimamo wake dhidi ya urasimu na utendaji hafifu, Mwalimu amesisitiza kuwa viongozi watakaoteuliwa kama wakuu wa mikoa au wilaya hawatakuwa ‘machawa’ bali watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa matokeo.

“Ukiteuliwa mkuu wa mkoa, sitaki uchawa. Niletee ripoti ya kazi, siyo sifa. Vinginevyo, milango ipo wazi, tupishane,” amesema.


Akiwataja wafanyabiashara kutoka nchi jirani, Mwalimu amesema si sahihi kwao kusafiri hadi Dar es Salaam kwa ajili ya bidhaa ilhali Uyole inaweza kubadilishwa kuwa “Congo ndogo” yaani kitovu cha kanda kwa biashara na usafirishaji wa bidhaa.

 “Kwa nchi inayojitambua, makutano kama ya Uyole hayawezi kuwa hovyo hivi. DR Congo anaweza kuishia hapa inakuwaje inaruhusu mtu anafika Dar es Salaam, lakini bidhaa bado zinapitia mbali. Kwa nini isiwe Uyole?” amehoji.

Mwalimu amekosoa serikali ya sasa kwa kutelekeza makutano hayo ya kimkakati akisema kama serikali ingejikita kwenye ujenzi wa miundombinu bora, eneo hilo lingeweza kuinua uchumi si tu wa Tanzania, bali pia wa nchi jirani.

“Kama kweli tunataka maendeleo, Uyole lazima ibadilishwe. Hatuwezi kuendelea kukumbatia sera zilezile za zamani za ujamaa na kujitegemea zisizotoa matokeo ya kisasa,” amesema

Katika hatua nyingine ameahidi kujenga barabara ya njia sita kutoka Uyole, Mbeya hadi Tunduma, mkoani Songwe, endapo atachaguliwa kuwa rais.

Amesema barabara hiyo ni ya kimkakati na ilistahili kujengwa miaka 25 iliyopita, lakini Serikali ya sasa imeshindwa kutekeleza hilo.

 “Hii barabara ilitakiwa kujengwa miaka 25 iliyopita na wala si leo. Nawahakikishia wananchi wa Uyole na Mbeya kuwa nikishinda, barabara hii nitaijenga kwa kuwa naamini katika barabara za kimkakati. Kutoka hapa Uyole hadi Tunduma ni lazima iwe ya njia sita na si nne,” amesema Mwalimu.

Amefafanua kuwa kati ya njia hizo sita, mbili zitakuwa mahsusi kwa malori na mbili kwa magari ya kawaida, hatua itakayosaidia kupunguza msongamano mkubwa wa magari na malori unaojitokeza mara kwa mara katika eneo hilo.

Mwalimu amesema uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji utafungua fursa za uwekezaji wa majengo na biashara, na hivyo kupunguza msongamano wa watu na shughuli Dar es Salaam.

Kwa upande wa sera, Mwalimu amesema Chaumma kinalenga kujenga uchumi wa kisasa, tofauti na sera za chama tawala, ambazo amedai kuwa zimepitwa na wakati.

“Sisi tunaamini katika uchumi wa kisasa na mipango ya maendeleo inayozingatia mabadiliko ya dunia, tofauti na CCM inayoendelea kushikilia sera ya ujamaa na Kujitegemea,” amesema.

Mgombea ubunge wa Uyole kupitia chama hicho, Ipyana Njiku, ameibua matumaini mapya kwa wakazi wa jimbo hilo baada ya kuahidi kushughulikia changamoto kubwa zinazolikumba eneo hilo endapo atapewa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao bungeni.

Njiku amebainisha kuwa jimbo hilo linakabiliwa na matatizo kadhaa ya miundombinu, yakiwemo barabara duni, ukosefu wa soko la kisasa, na kutokuwepo kwa stendi rasmi ya mabasi ambayo inakwamisha shughuli za usafiri na biashara.

Mgombea huyo ameahidi kuwa, akipewa nafasi ya kuwa mbunge, atahakikisha anashirikiana na mamlaka husika kufanikisha ujenzi wa barabara bora, ujenzi wa soko la kisasa, pamoja na stendi ya mabasi ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jimbo hilo.

Njiku amewataka wananchi wa Uyole kumchagua kwa imani kuwa ataibeba sauti yao na kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu kupitia ushawishi wa kisera bungeni.

“Ninakuja si kwa maneno, bali kwa dhamira ya kweli ya kuwatumikia. Maendeleo hayawezi kupatikana bila miundombinu bora. Tukishirikiana, tutabadili sura ya Uyole,” amesema.