Ndoto ya Ndugai ujenzi hoteli ya nyota tano Dodoma yatimia

Dodoma. Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika (CPA Africa Region), kimeingia mkataba wa miezi 22 na kampuni ya CRJE East Africa Limited kwa ajili ya ujenzi wa hoteli ya nyota tano jijini Dodoma itakayokuwa  hoteli ya kwanza ya aina hiyo katika jiji hilo.

Hoteli hiyo, itakayoendeshwa na kampuni ya Pristine and Time, inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 22 kuanzia sasa.

Wazo la kujenga hoteli hiyo lilibuniwa mwaka 2019 na aliyekuwa Spika wa Bunge wakati huo, hayati Job Ndugai.

Hata hivyo, utekelezaji wake uliahirishwa kwa muda kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba huo iliyofanyika Bungeni, Dodoma, Septemba 26, 2025, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk Tulia Ackson, amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika kwa wakati.

Dk Tulia amesema ujenzi huo utaongeza uwezo wa Jiji la Dodoma kuhudumia wageni wa kimataifa, hasa wakati wa mikutano ya kimataifa, kwa kuwa hoteli hiyo itakuwa na vyumba maalumu kwa ajili yao.

“Wageni kutoka nje ya nchi hawatalazimika kuondoka siku hiyohiyo ya tukio. Watakuwa na sehemu rasmi ya kufikia na kulala, jambo litakaloongeza hadhi ya jiji letu kimataifa.

“Dodoma ni makao makuu ya nchi na makao makuu ya Bunge letu, kwa hiyo wageni wote wa Rais na wa Bunge watakuwa wanafikia kwenye hoteli hiyo hawatalazimika kuja na kuondoka siku hiyohiyo kwa kuwa kutakuwa na vyumba maalumu vya kuwalaza,” amesema Dk Ackson.

Pia, amesema kukamilika kwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato kutarahisisha ujio wa wageni wa kimataifa nchini, ambao watapata huduma ya malazi katika hoteli hiyo ya nyota tano.

Aidha, amesema wazo la kujenga hoteli hiyo liliasisiwa mwaka 2019 na aliyekuwa Spika wa Bunge wakati huo, Job Ndugai (kwa sasa ni marehemu), lakini utekelezaji wake ulisuasua kutokana na ukosefu wa fedha.

Hata hivyo, sasa Benki ya CRDB kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kifedha imewezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi huo.

Kwa upande wake, Katibu wa Bunge, Baraka Leonard amesema hoteli hiyo itajengwa katika eneo la Njedengwa, ambapo Serikali ililitenga rasmi eneo hilo pamoja na kutoa vibali vyote vinavyohitajika.

Amesisitiza kuwa hoteli hiyo ni sehemu ya mradi wa kitega uchumi wa CPA Kanda ya Afrika.

Leonard ameongeza kuwa mkataba wa ujenzi wa hoteli hiyo ni wa miezi 22, na wana matumaini kuwa ujenzi utakamilika kwa wakati ili hoteli ianze kutoa huduma kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake, Mweka Hazina wa CPA Kanda ya Afrika, mbunge kutoka Uganda, Enosy Asiimwe amesema mradi huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wanachama wa CPA, na hautakuwa wa hasara bali wa faida endelevu.

Amesema Tanzania imechaguliwa kuwa mahali pa mradi huo kwa kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndilo makao makuu ya CPA Kanda ya Afrika.