Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema mfumo wa elimu utakaoundwa na serikali ya chama hicho utawezesha wanafunzi wa Zanzibar kushindana na si kuwa wasindikizaji.
Amesema ACT-Wazalendo ikishika madaraka katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 imedhamiria kuhakikisha Zanzibar inakuwa Taifa lililoelimika ili kuendana na hali ya sasa na baadaye.
Ameeleza hayo leo Jumamosi Septemba 27, 2025 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mzee Mgeni, Jimbo la Pangawe, Mjini Unguja akiendelea kusaka kura za urais, wabunge, wawakilishi na udiwani.
“Mfumo tulionao sasa tutabaki kuwa wasindikizaji, watoto wetu watabaki kuwa wasindikizaji. Hatutaki hilo litokee Zanzibar, bali tunataka watoto wetu kushiriki katika uchumi wa dunia ili kujisikia fahari ya kuzaliwa Zanzibar,” amesema na kuongeza:
“Ili kujisikia fahari ya kuzaliwa Zanzibar, lazima tuwajengee misingi ya elimu itakayowawezesha kushinda na dunia.”

Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, ameahidi pia kutoa kompyuta mpakato kwa wanafunzi wa sekondari wa Zanzibar ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kusoma na kujifunza, akisema mchakato huo unawezekana.
“Tutaanzisha miji ye elimu ili kutengeneza mazingira ya watu kujifunza kwa urahisi, kubadilishana mawazo. Tumeshachagua maeneo ya kuanzisha miji hii, ACT ni kama askari tukitua tunaanza kazi,” amesema.
Mkazi wa Pangawe, Fatma Khamis amesema: “Hii ni mara ya kwanza tunasikia mgombea kuahidi kutoa laptop (kompyuta mpakato), endapo litafanikiwa vijana wetu hawatabaki nyuma na teknolojia.”
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Zanzibar), Ismail Jussa, amesema watumishi wa umma wa Zanzibar kulipwa kima cha chini cha mshahara wa Sh1 milioni ni jambo linalowezekana, akiwataka wananchi kupuuza yanayosemwa kwamba haiwezekani.
“Imekuwa nongwa Othman kuahidi Sh1 milioni ya mshahara kwa mwezi kwa watumishi wa umma, mara oooh… haiwezekani, labda ninyi mliokaa madarakani kwa muda mrefu hamuwezi, lakini si ACT-Wazalendo,” amesema na kuongeza:
“Tukijaaliwa Oktoba 29, tunamwapisha Rais wetu Othman, kisha tunawapa neema wafanyakazi wa Serikali ambayo ninyi imewashinda kwa miaka 48,” amesema.
Jussa amesema kila kilichoahidiwa na ACT-Wazalendo, kimefanyiwa utafiti wa kina na siku chache zijazo watazindua ilani ya uchaguzi ya chama hicho ili kufafanua kwa kina hoja na ahadi zao.
Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, ACT-Wazalendo, Salim Biman, amewataka wanachama wa chama hicho, kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba ili kumuongezea kura Othman.
“Huyu ni mgombea wetu, lazima tubebe hii kampeni ya nyumba kwa nyumba, mtu kwa mtu. Kila mtu amfanyie kampeni Othman, kila mtu angalau awe na kura 10 mkononi,” amesema.