Pamba Jiji vs TRA United ni vita ya makocha Wakenya

KESHO kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, kuna mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya wenyeji Pamba Jiji dhidi ya TRA United kutoka Tabora kuanzia saa 8 mchana.

Mechi hiyo inatarajiwa kuvuta hisia za watazamaji wengi kutoka na kukutanisha makocha wawili wa timu hizo ambao ni raia wa Kenya. Francis Baraza wa Pamba Jiji na Kassim Otieno upande wa TRA United. Mbali na hilo, timu zote zinasaka ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Hiyo itakuwa ni mechi ya tatu kwa timu hizo kukutana tangu msimu uliopita, ambapo kila moja imeibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Msimu huu haujaanza vizuri kwa timu zote. Pamba Jiji imeambulia sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Namungo FC, kisha kuchapwa mabao 3-0 na Yanga SC, huku TRA United ikianza kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema anaamini vijana wake wana nafasi kubwa ya kuondoka na ushindi kesho kutokana na maandalizi waliyofanya.

“Tunapofanya mazoezi unaona morali, jambo ninalosema ni kwamba vijana wangu wabebe kile tunachokifanya mazoezini wakilete kwenye mchezo wa kesho bila shaka tunaweza kuondoka na ushindi,” amesema Baraza.

Ameongeza kuwa faida kubwa kwao ni kucheza mchana kwa sababu ndicho kipindi ambacho wamezoea kufanya mazoezi.

“Ni muda mzuri ambao pia mashabiki watapata nafasi ya kuona kile wanachokitarajia kutoka kwetu, kwa hiyo naona ni nzuri kwetu kwa sababu hatujazoea kucheza usiku,” amesema Baraza.

Nyota wa Pamba Jiji, John Nakibinge amesema kikosi kipo tayari na morali iko juu kuelekea mchezo huo.

Sisi kama wachezaji tumesafiri kutoka Dar na tunaweza kusema tuko tayari. Mwalimu ameshatuandaa na kesho tunaingia kuhakikisha kwamba Pamba inapata alama tatu za mwanzo wa msimu.

“Michezo miwili iliyopita matokeo tuliyopata na pongezi tulizopokea kwa namna tulivyocheza zimetupa motisha kwamba kuna kitu kizuri kinafanyika, kwa hiyo kesho tunataka tuendeleze kile tulichoanza nacho na kuongeza zaidi,” amesema Nakibinge.

Kocha wa TRA United, Kassim Otieno amesema wametumia wiki moja kujiandaa na mchezo huo na kuwasoma wapinzani wao wanavyocheza, hivyo, wako tayari kupata pointi tatu.

Amesema wamefanyia kazi makosa ya mechi ya kwanza na wataingia kwa tahadhari dhidi ya Pamba Jiji.

“Kama mechi ya kwanza tulifunga mabao mawili basi mechi ya pili tunaweza pia kuzuia tusifungwe, kwa hiyo unaweza kuona wiki nzima tumejaribu kuona namna gani tunaweza kuzuia na jinsi ya kufunga mabao, hivyo tumejiandaa vizuri kuondoka na matokeo chanya,” amesema Otieno.

Otieno amesema wanaheshimu ubora wa wapinzani wao, lakini wako tayari kumudu presha ya mechi hiyo.

“Lazima tuje na tahadhari kwa sababu ukiwaangalia wapinzani wetu ni timu nzuri sana, wana wachezaji wengi wenye uzoefu na sisi tuko ugenini lazima tuwe makini namna tunavyocheza nao na itabidi tufanye kazi ya ziada kwa sababu watakuja na presha wakihitaji ushindi, hivyo tumejaribu kuzingatia hayo na tuko tayari kumudu hiyo presha,” amesema Otieno.

Akimzungumzia kocha mwenzake Francis Baraza, Otieno amesema kila mmoja ana falsafa yake ya ufundishaji na mechi ya kesho itaonesha nani atakuwa na mbinu bora za ushindi.

“Kuna tofauti kubwa ya kiufundishaji kati yangu na Baraza kwa sababu yeye ni makocha wale waliotangulia na mpira umekuwa wa kisasa.

“Kwa hiyo mechi ya kesho tutaona utofauti kati yangu na kocha Baraza kwa upande wa uchezaji na mbinu, lakini hakuna upinzani ama uhasama wowote. Mimi hapa nimekuja tu kucheza mechi tutoke na pointi tatu na siyo kushindana,” amesema Otieno.

Kiungo wa TRA United, Emmanuel Mwanengo amesema kikosi kipo tayari na morali iko juu kuelekea mtanange huo.

“Kwa upande wa maandalizi mimi na wachezaji wenzangu tumesafiri na kufika hapa salama na kila mchezaji ana hali nzuri na morali kwa ajili ya mchezo wa kesho,” amesema Mwanengo.

Amesema matokeo ya mechi ya kwanza yamewapa hamasa ya kupambana zaidi kesho dhidi ya Pamba Jiji.

“Mchezo wa kwanza tuliumizwa na matokeo ya sare ya 2-2 dhidi ya Dodoma Jiji tukiwa nyumbani. Hii ilichangia kwa sababu asilimia 90 ya kikosi ni wachezaji wapya, kwa hiyo tulihitaji muda wa kuzoeana, lakini tunaamini katika mchezo wa kesho tutafanya vizuri,” amesema Mwanengo.