Richkard azitaka alama tatu Pemba 

Kocha Msaidizi wa Malindi, Mohamed Salah ‘Richkard’ amesema timu hiyo imejipanga vyema kuhakikisha inazipata pointi tatu za kwanza katika Ligi Kuu Zanzibar.

Mechi hiyo itachezwa leo Jumamosi saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, ambapo Chipukizi itakuwa mwenyeji wa Malindi.

Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo, Richkard amesema kutumia wachezaji wapya katika mechi hiyo sio sababu ya kuzikosa alama ambazo ni muhimu kwao.

Ameeleza kuwa, zipo dhana kwamba wachezaji wakiwa bado wapya wanashindwa kuwa na mawasiliano mazuri uwanjani jambo ambalo analiona sio sahihi kwake.

“Wachezaji wa mpira siku moja tu inatosha kuelewana na hasa wa timu yetu kwa sababu tumechukua wachezaji wenye vipaji na misingi ya kimpira kutoka nchi tofauti,” amesema.

Kikosi hicho kiliondoka Uguja juzi kuelekea kisiwani Pemba kwa ajili ya mechi hiyo ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Zanzibar.

Ligi hiyo iliyoanza Septemba 25 mwaka huu, jana Ijumaa Zimamoto iliizima Junguni United kwa kuiangushia kichapo cha mabao 2-0.