Ngorongoro. Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau katika kukuza sekta ya utalii, ambayo kwa mwaka 2024 imeingizia Taifa Dola za Marekani bilioni 3.9 (sawa na Sh9 trilioni).
Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi, amesema hayo jana Septemba 27, 2025 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani yaliyofanyika katika eneo la Ngoitokitoki, Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Alisema sekta hiyo imechangia ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi, huku idadi ya watalii wa kigeni ikipanda kutoka 922,000 mwaka 2021 hadi kufikia milioni 2.14 mwaka 2024, na wa ndani kutoka 788,000 hadi milioni 3.12 katika kipindi hicho.
“Sekta ya utalii mwaka 2024 ndiyo imekuwa namba moja nchini kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Hii sekta inapoanguka, nyingine zote huathirika,” amesema.
Dk Abbasi amesema zaidi ya watu milioni 2.5 wameajiriwa katika mnyororo wa sekta hiyo, huku Serikali ikitenga asilimia 32 ya ardhi ya nchi kwa ajili ya hifadhi, mapori ya akiba, misitu na malikale.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuipa Tanzania heshima kimataifa kupitia tuzo mbalimbali za utalii, ikiwemo kushinda tuzo ya safari bora duniani.
“Kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu, sekta ya utalii imekua kwa asilimia 10 na takwimu rasmi zitawasilishwa mwisho wa mwaka,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Abbasi ametangaza kuwa Desemba 19 mwaka huu kutatolewa tuzo za pili za uhifadhi, ambapo zaidi ya tuzo 56 zitatolewa katika makundi saba.
Amesema baadhi ya tuzo zitapigiwa kura na nyingine kuamuliwa na majaji, huku wakaguzi wa nje wakihusishwa ili kuhakikisha washindi wanakidhi vigezo, akifananisha mfumo huo na tuzo za kimataifa za Oscar na Grammy.
Mmoja wa waongoza utalii, Dunstan Julius, amesema hatua za Serikali kushirikiana na wadau zinaboresha sekta hiyo na kutoa nafasi nyingi za ajira.
“Tunaomba ushirikiano huu uendelee kwani sekta ya utalii inapunguza tatizo la ajira na vijana wengi wanajiajiri kupitia shughuli za kiutalii,” amesema.