OFISA Habari wa Simba, Ahmed Ally, amesema wana mechi ngumu kesho watakapokutana na timu ambayo haina cha kupoteza, hivyo wapo kwenye wakati mgumu kufikiria nini watafanya ili kuvuka hatua inayofuata.
Katika kufikiria huko, Ally amebainisha kwamba, wataingia kwenye mechi hiyo akilini mwao matokeo yakiwa 0-0 licha ya kwamba ugenini walishinda bao 1-0.
Kesho Jumapili, Simba itakuwa mwenyeji kwenye mechi hiyo ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali dhidi ya Gaborone United ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini.
“Bao moja tulilolipata tumelifuta, hatuwezi kulitegemea, kwenye akili zetu mechi ya kesho ni bila bila ili kujipa nguvu ya kupambana kuhakikisha tunafika nchi ya ahadi.

“Mechi sio nyepesi hata kidogo, tuna kila sababu ya kuwekeza nguvu kubwa ili kupata matokeo mazuri na hatimaye kutinga hatua inayofuata, licha ya kutokuwa na nafasi ya kuingiza mashabiki, tunahitaji maombi yenu,” amesema Ally.
Katika hatua nyingine, Ally amewaita mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishuhudia mechi hiyo katika Fukwe za Coco Beach baada ya Mwembe Yanga.

“Kuna mabadiliko kidogo, mwanzo tulipanga kuweka TV kubwa Mwembe Yanga, lakini kutokana na uwepo wa masuala ya kisiasa eneo hilo litakuwa na jukumu la kampeni, hivyo tutakuwa Coco Beach, karibuni Wanasimba mshuhudie timu yenu ikifikia malengo ya kutinga hatua inayofuata,” amesema Ally.