Tanzania Yapata Medali ya Dhahabu Apimondia 2025

Tanzania imepata heshima kubwa ya kimataifa baada ya kutunukiwa Medali ya Dhahabu katika Kongresi ya 49 ya Apimondia iliyofanyika katika ukanda wa Scandinavia (Sweden, Denmark na Norway).

Tuzo hiyo ilitangazwa Septemba 27, 2025 ambapo banda la Tanzania lilishinda katika kipengele cha Large Stand (zaidi ya mita 36 za mraba) kutokana na ubunifu na ubora wa maonesho ya mazao ya nyuki yaliyovutia wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Cheti cha ushindi kimetolewa na Rais wa Shirikisho la Apimondia, Jeff Pettis, kwa kutambua mchango wa Tanzania katika kukuza tasnia ya nyuki kimataifa.

Akizungumza mara baada ya kupokea cheti hicho, Kamishna Msaidizi anayesimamia Rasilimali za Nyuki, Hussein Msuya, alisema ushindi huo ni ishara kuwa Tanzania imeanza kuthibitisha nafasi yake kama kitovu cha uzalishaji na usindikaji wa mazao ya nyuki barani Afrika na duniani.

“Ushindi huu unatarajiwa kuongeza thamani ya bidhaa za nyuki za Tanzania sokoni, hususan asali, nta na chavua, na hivyo kuwaongezea kipato wakulima na wajasiriamali wadogo,” alisema Msuya.

Washiriki kutoka Tanzania walisema medali hiyo ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya Serikali, wadau wa sekta binafsi na wafugaji nyuki walioweka mbele ubora, uendelevu na matumizi bora ya rasilimali za misitu na nyuki nchini.