TRA yajizatiti huduma kwa wafanyabiashara wadogo

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wadogo na wa kati mkoani Dar es Salaam wametakiwa kuchangamkia dawati la uwezeshaji biashara lililozinduliwa likilenga kuimarisha biashara zao.

Dawati hilo limezinduliwa leo Septemba 27, 2025 na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Dawati hilo linalenga kutoa huduma muhimu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, zikiwamo za elimu ya biashara, mikopo, masoko na fursa nyingine zinazoweza kuongeza ufanisi wa biashara zao.

Mwenda amesema sekta ya biashara ni nguzo muhimu katika ukusanyaji wa kodi, ndiyo maana TRA inaweka mikakati ya kuunga mkono wafanyabiashara.

Amesema dawati hilo litaenda sambamba na juhudi za TRA kutatua changamoto za wafanyabiashara.

“Tunazindua dawati hili kwa sababu Mkoa wa Dar es Salaam unachangia asilimia 80 ya mapato ya kodi nchini. Hivyo, ni muhimu kuimarisha biashara na kumsaidia mfanyabiashara aweze kuongeza ufanisi,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema dawati hilo ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara wadogo, hasa katika sekta zinazohusiana na bodaboda, mama lishe na machinga.

“Dawati hili litachochea ukuaji wa biashara ndogo na kuhakikisha wanapata fursa za mikopo, masoko na hata kuelimishwa kuhusu kulipa kodi,” amesema.

Amesema wilaya hiyo imetenga Sh16 bilioni kwa ajili ya mikopo ya wafanyabiashara wadogo, hivyo dawati hilo litawasaidia kupata huduma kwa urahisi na haraka.

Kamishna wa kodi za ndani, Godwin Balongo, amesema: “Dawati hili linatarajiwa kutoa huduma kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati na litakuwa na manufaa makubwa kwa sekta ya biashara nchini.”

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, Sevelin Mushi, ametoa wito kwa TRA kuhakikisha dawati hilo  linakuwa msaada kwao badala ya kuwa kikwazo.

Amesema wanakabiliwa na changamoto ya kulipa kodi akiitaka TRA kupunguza mzigo huo.

Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Taifa, Steven Lusinde, amesema dawati hilo ni dawa ya kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wadogo na wa kati.