YANGA imefuzu hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifunga Wiliete SC ya Angola kwa mabao 2-0 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 5-0, huku maswali ya mashabiki kuhusu ubora wa kiwango cha timu hiyo ya Wananchi yakiendelea kuwa mengi.
Kwa ushindi huo, Yanga itakabiliana na Silver Strikers ya Malawi kuwania kufuzu hatua ya makundi katika mechi yao ya hatua ya pili ya mtoano.
Licha ya baadhi ya mashabiki kutovutiwa na kiwango ambacho kikosi cha timu hiyo kinachobadilishwa badilishwa na kocha mpya Romain Folz, timu imeendelea kuwa mwendo mzuri wa ikishinda mecho zote tano ilizocheza msimu huu tena bila ya kuruhusu bao.
Iliifunga Bandari Kenya 1-0 katika mechi ya kirafiki ya kilele cha tamasha la Wiki ya Mwananchi, ikaifunga Simba 1-0 na kutwaa Ngao ya Jamii, ikaibwaga Wiliette 3-0 ugenini Angola kisha ikaibwaga Pamba Jiji 3-0 katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara na jana ikailaza tena Wiliette 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Matokeo hayo ya kushinda mechi zote tano mfululizo bila ya kuruhusu bao imewafanya baadhi ya mashabiki kuwaambia wenzao ‘tulieni, kuleni mtori, nyama mtazikuta chini.”
Ushindi wa mabao 3-0 ilioupata ugenini dhidi ya Wiliete nchini Angola, kwa kiasi kikubwa uliwapa nguvu ya kuingia uwanjani jana na kupata ushindi mwingine wa mabao 2-0 ulioivusha Yanga kwa jumla ya mabao 5-0 ikiisaka hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa msimu wa tatu mfululizo.
Katika mechi ya jana iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kocha wa Yanga, Folz alifanya mabadiliko ya kikosi kutoka kile kilichocheza ugenini nchini Angola, wiki iliyopita.
Kikosi alichoanza nacho jana kilikuwa na maingizo mapya manne ambayo ni Kibwana Shomari, Dickson Job, Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya. Akiwaacha Israel Mwenda, Bakari Mwamnyeto, Clement Mzize na Mohamed Doumbia.

Yanga ilisubiri hadi dakika ya 70 kupata bao lililofungwa na Pacome Zouzoua ambaye aligongeana pasi na Andy Boyeli kabla ya kumchambua kipa na kuuweka mpira kimiani.
Baada ya kuingia bao hilo, hali ya furaha ilionekana kwenye benchi la ufundi la Yanga hata majukwaani ambapo mashabiki walishangilia kwa nguvu.
Kabla ya kuingia bao hilo, Yanga ilitengeneza nafasi chache za kufunga huku Wiliete nayo ikijibu mapigo, lakini hakuna aliyetumia vizuri makosa ya mpinzani wake.
Kipindi cha kwanza kilichomalizika kwa matokeo ya 0-0, kilikuwa na mashambulizi ya hapa na pale ambapo ilibaki kidogo Wiliete iandike bao kwani kichwa kilichopigwa na Junior mpira uligonga mwamba na kurudi uwanjani huki kipa Djigui Diarra akishindwa la kufanya.
Aziz Andabwile akaongeza bao la pili dakika ya 86 kwa kichwa akiunganisha kona iliyopigwa na Offen Chikola.
Ushindi huo unaifanya Yanga kwenda kukutana na Silver Strikers hatua ya pili ya michuano hiyo ambapo mchezo wa kwanza utafanyika nchini Malawi kati ya Oktoba 17 na 19, kisha marudiano jijini Dar es Salaam kati ya Oktoba 24 na 26 mwaka huu.
Silver Striker nayo imefuzu hatua hiyo baada ya kuiondosha Elgeco Plus ya Madagascar kwa bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1. Mechi ya kwanza iliyochezwa Madagascar, ilimalizika kwa sare ya 1-1, na ziliporudiana jana huko Malawi ikawa 0-0.
Wakati huohuo, Mlandege ya Zanzibar imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ethiopia Insurance katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini imeshinndwa kusonga mbele kufuatia ugenini kufungwa 2-0 na matokeo ya jumla kuwa Mlandege 3-4 Ethiopia Insurance.

YANGA: Djigui Diarra, Kibwana Shomari, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Aziz Andabwile, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Prince Dube, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua.
WILIETE: Agostinho Calunga, Wiwi, Giovani Chipopolo, Felipe, Mule, Danilson, Skudu Makudubela, Giovani, Ning, Junior, Quare, Cesar Cangue.