Dodoma. Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar, Augustino Shao amesema amani ya kweli haiwezi kupatikana bila haki, akisisitiza kwamba mioyo ya watu wengi inavuja kwa kukosa haki licha ya kuonekana wametulia.
Askofu Shao amesema hayo leo leo Jumapili Septemba 29, 2025 wakati akihubiri kwenye misa ya Sakramenti ya Kipaimara, katika Parokia ya Kivule, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Kauli hiyo ya Askofu Shao ni mwendelezo wa hoja ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali nchini, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, kuhusu umuhimu wa haki na amani nchini.
Machi 2025, viongozi wa dini ya Kiislamu walieleza umuhimu wa kusimamia haki, demokrasia na kuepuka rushwa ili kuwapata viongozi watakaowawakilisha wananchi na kuendeleza maadili mema yaliyokuwa yakifanyika kwenye mfungo wa Ramadhani.
Akizungumza kwenye misa hiyo, Askofu Shao amesema hakuna amani kama hakuna haki akibainisha kwamba watu wengi wanaweza kuwa wamenyamaza lakini mioyo yao inavuja kwa kukosa haki.
“Mtu ambaye amenyimwa haki yake lakini hapigani si tutasema ana amani japo amenyimwa haki yake? Ukimwangalia moyo unavuja kwa kukosa haki yake. Haki ndiyo msingi wa amani ya kweli, si kutokuwa na vita ndipo tunazungumzia amani,” amesema.
Amesema kwa wakati huu wa uchaguzi, suala la haki na amani ni msingi mkuu, ambao kila mmoja angetamani kufahamu na kuelezwa.
“Tunawaweka wakfu kwa ajili ya kazi maalumu ili mkawe wakweli, wenye haki, wanaotetea haki na kuiishi haki ambayo inajenga amani duniani.
“Sisi Tanzania tunazungumzia haki na amani na ndiyo maana sasa tunazungumzia uchaguzi wa amani, lakini sisi kanisa tunasema hakuna amani ya kweli kama hakuna haki, mnanielewa?” amehoji askofu huyo.
Askofu Shao amesema yeye hapigi siasa, isipokuwa anataka waumini, wazazi na vijana waliopata Kipaimara watambue namna wanavyopaswa kuipata haki bila kuwa na kivuli cha amani.
Kauli ya Askofu Shao ambayo si mara ya kwanza kutolewa na viongozi wa kanisa hilo, inakuja katika kipindi ambacho kumekuwa na mawazo tofauti na madai ya kukosekana uwanja sawa kwenye uchaguzi kutokana na mifumo iliyopo ya kisheria na kikatiba.
Vilevile, kumekuwepo malalamiko ya baadhi ya wanasiasa kukosa haki kugombea, baadhi yao wakia wameongoza kwenye kura za maoni.
Suala la haki kwenye uchaguzi limekuwa wimbo unaoimbwa kila uchaguzi licha ya kuwepo baadhi ya mabadiliko ya sheria.
Miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa yanalalamikiwa ni muundo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa bado imelalia upande mmoja.
Mwanasiasa wa siku nyingi na makamu mwenyekiti mstaafu wa Chama cha ukombozi wa Umma (Chaumma), Kayumbo Kabutali amesema kauli ya Askofu Shao ni sahihi na imekuja kwa wakati sahihi.
Kabutali amesema mahubiri ya amani yapo kila kona na watu wengi wanaamini hilo, lakini neno haki kutoka kwa watawala halitamkwi kabisa.
Amesema ndimi za watawala hazitamki haki na masikio ya walio wengi hayapendi kusikia neno haki zaidi ya mdundo wa amani kwenye ngoma za masikio.
“Hawa wenzetu wanasema wamefanya mambo makubwa, lakini ukweli tunapitia magumu sana sisi wa vyama vingine, hakuna haki na bado haijapatikana, labla itokee miujiza sasa,” amesema.
Kabutali ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Mtumba mkoani Dodoma, amelalamika kuwa hata kwa wagombea wanaotoka vyama vya upinzani kumekuwa na kilio kikubwa cha kutafuta haki, japo wanaambiwa wapo katika nchi yenye amani.
Katekista wa Kanisa la Anglikana na Diwani mstaafu, Joseph Mbula amesema mahubiri ya askofu ni maono ya kiroho lakini hayapaswi kutafsiriwa kama hakuna haki.
Mbula amekiri kwamba ni kweli haki inaendana na amani, ambavyo ni kulwa na doto, lakini si tafsiri ya mahubiri ya leo.
“Pale Askofu alikuwa anazungumza na waumini, wazazi na watoto waliopata Kipaimara na ndiyo maana amesema hafanyi siasa pale,” amesema.
Hata hivyo, kiongozi huyo amesisitiza kauli za viongozi wa dini kwa sasa zinapaswa kuangaliwa zaidi kwani zinaweza kuwa kwenye mitazamo miwili tofauti, kama wanavyodhani watu au kinyume chake.