SAA mbili na nusu asubuhi niliwasili kwenye nyumba namba 313 iliyokuwa eneo la Chuda. Ilikuwa ni asubuhi ya siku ya pili, ambapo jana yake tulikwenda katika hospitali ya Muheza kuzungumza na askari mstaafu aliyetupa siri ya kuachiwa kwa kina Unyeke.
Mtu tuliyekuwa tunamtuhumu kuhusika na mauaji ya kina Unyeke, Thomas Christopher, aliandikisha katika usajili wa laini yake ya simu kuwa alikuwa akiishi katika nyumba hiyo.
Nilishafika mara mbili kwenye nyumba hiyo kumuulizia, na mara ya pili msichana niliyekuwa ninakutana naye aliniahidi kunipatia namba ya simu ya mwenye nyumba hiyo.
Niliamua kuwahi kufika mapema ili nimpate mume wake ambaye niliambiwa ndiye aliyekuwa na namba hiyo.
Wakati nafika, niliona geti limefunguliwa na gari lilikuwa linatoka. Pembeni mwa geti alisimama yule msichana niliyekuwa ninazungumza naye. Nikahisi yule aliyekuwa anatoka na gari ndiye mume wake. Kwa kuhofia kwamba anaweza asisimame akaendelea na safari, nilisimamisha gari mbele ya gari lake.
Baada ya kuona kulikuwa na gari lililosimama mbele ya gari lake, akafunga breki.
Nilifungua mlango nikashuka na kumfuata.
Alikuwa kijana mnene na mfupi aliyevaa miwani ya macho.
“Habari yako?” nikamsalimia.
“Nzuri,” akanijibu kwa mkato huku akinitazama kwa macho ya tashwishi.
Nikamtazama mke wake naye nikamsalimia.
“Habari ya tangu jana?”
“Nzuri. Jana hukurudi tena,” akaniambia.
“Nilitingwa na kazi nikashindwa kuja. Nimeamua nije leo.”
“Mume wangu ndiye huyo aliyeko kwenye gari. Nilimwambia, akaniambia nikupe namba yake umpigie, lakini kwa vile mmekutana atakupa mwenyewe.”
“Ndiwe wewe uliyekuwa unataka namba ya mwenye nyumba hii?” kijana huyo akaniuliza.
“Ndiyo, ni mimi.”
“Nilishindwa kumpa huyu bibi hiyo namba kwa sababu nilikuwa sijakuelewa. Ngoja nikupatie.”
Kijana huyo alitoa simu yake akanitajia namba hiyo. Niliiandika kwenye simu yangu kisha nikamuuliza:
“Anaitwa nani?”
“Huyu mama anaishi Iringa, anaitwa mama Rachel au mama Recho.”
Wakati naliandika jina hilo, kijana huyo akaniuliza:
“Kuna tatizo gani?”
“Kuna mtu ninamtafuta. Niliambiwa anaishi katika nyumba hii.”
“Ni nani?”
“Anaitwa Thomas Christopher.”
Kijana huyo akatikisa kichwa.
“Hatumfahamu. Labda kama alikuwepo kabla ya sisi kuhamia hapa.”
“Ndiyo sababu nilitaka kupata namba ya mwenye nyumba ili atufahamishe kama anamfahamu.”
“Sawa. Mpigie umuulize.”
“Nitakwenda kumpigia ofisini. Asanteni sana.”
Nilipowambia hivyo, nikaondoka nikaenda kujipakia kwenye gari na kuliondoa. Nilirudi ofisini.
Baada ya kukaa kwenye kiti niliipiga ile namba.
Namba ikaita. Baada ya sekunde chache ikapokewa na sauti ya mwanamke ikasikika ikisema:
“Hello!”
“Hello! Habari ya asubuhi?”
“Nzuri, sijui wewe?”
“Mimi ni mzima. Unazungumza na mtu mmoja kutoka Tanga. Namba yako nilipewa na mpangaji wako wa Chuda.”
“Ulikuwa na tatizo gani?”
“Nilikuwa namhitaji Thomas Christopher.”
“Thomas Christopher?”
“Ndiyo.”
“Unamkusudia Thomas Christopher gani?”
“Ambaye aliwahi kuishi katika nyumba ile ya Chuda ambayo nimeambiwa ni mali yako.”
“Nadhani Thomas unayemkusudia wewe hivi sasa ni marehemu. Huyo kijana niliambiwa baba yake ndiye aliyekuwa na nyumba ile, lakini aliuawa.”
“Aliuawa lini?”
“Ni muda sana. Tangu mume wangu aliponunua nyumba hiyo ya Chuda imepita karibu miezi kumi. Wakati huo huyo kijana alikuwa ameshauawa na hata waliomuua walishakamatwa na kuhukumiwa kunyongwa na mahakama. Kwa hiyo utaona alikufa muda mrefu ingawa sijui alikufa lini.”
Nikaona mwanamke huyo alikuwa akinipa stori nyingine ambayo pia ilikuwa muhimu kwangu.
“Unasema mume wako ndiye aliyenunua hii nyumba?”
“Ndiyo.”
“Aliinunua kutoka kwa nani?”
“Aliinunua kutoka serikalini. Hizo ni miongoni mwa mali za huyo kijana aliyeuawa. Alipouawa hazikuwa na mrithi, zikachukuliwa na serikali.”
Wakati nazungumza na huyo mwanamke nilikuwa najiuliza kimoyomoyo, kama huyo kijana ameuawa kama ambavyo nilikuwa nafahamu, huyo aliyewanyonga kina Unyeke alikuwa nani?
“Unafahamu huyu kijana alizikwa wapi?”
“Sifahamu. Mimi naishi Iringa, mume wangu ndiye aliyekuwa Tanga naye pia alishafariki.”
“Nakushukuru dada yangu. Nitafanya utafiti kwa watu wanaomfahamu ili nijue alizikwa wapi.”
“Sawa kaka.”
“Nitakapokuwa na lolote la kukuuliza nitakupigia.”
“Sawa.”
Nikakata simu. Nilijiambia, kama kijana huyo alikuwa anaishi mahali hapo na akauawa, lazima majirani watafahamu mahali alipozikwa.
Nilipopata wazo hilo nikarudi tena Chuda. Nilikwenda kwenye nyumba moja iliyokuwa jirani na nyumba aliyokuwa akiishi Thomas. Mlango wa nyumba hiyo ulikuwa wazi.
Wakati nafika hapo nikamuona mzee mmoja akitoka.
“Shikamoo mzee,” nikamuamkia.
“Marahaba. Habari ya leo?”
“Nzuri. Mzee, nilikuwa na tatizo kidogo.”
“Tatizo gani?”
“Kuna kijana mmoja alikuwa akiishi katika nyumba hii kama mwaka mmoja au mmoja na nusu uliopita. Anaitwa Thomas Christopher.”
Nilimuonyesha ile nyumba aliyokuwa anaishi.
“Mbona huyo kijana alishakufa.”
“Ninajua kuwa aliuawa. Nilichokuwa ninakitaka ni kujua mahali alipozikwa.”
“Alizikwa hapa hapa Chuda. Kuna makaburi nyuma ya shule.”
“Sipafahamu.”
“Kwani wewe ni nani?”
Sikutaka kumdanganya, nikamtolea kitambulisho na kumuonyesha.
“Mimi ni afisa wa polisi, naitwa Inspekta Fadhil.”
“Ulikuwa unahitaji nini katika hilo kaburi?”
Lilikuwa swali gumu kidogo, lakini nilimjibu:
“Tunahitaji kujua mahali alipozikwa.”
“Naweza kukupeleka.”
“Nitakushukuru mzee. Nina gari na tunaweza kwenda mara moja halafu nitakurudisha.”
Wakati mzee huyo anajipakia kwenye gari aliniambia:
“Mahali penyewe ni karibu, tungeweza kwenda bila ya gari.”
“Si kitu, kwa vile gari lipo acha twende mara moja.”
Mzee huyo alinipeleka nyuma ya shule moja ya msingi ambako kulikuwa na eneo dogo la makaburi.
Tuliposhuka kwenye gari, mzee alikwenda moja kwa moja katika kaburi moja na kuniambia:
“Kaburi lake ni hili hapa. Ninalijua vizuri kwa sababu nilikuja kumzika.”
Nilimfuata yule mzee aliyekuwa amesimama kando ya kaburi hilo. Nilipofika karibu yake akaniambia:
“Ngoja nihakikishe.”
Alikwenda mbele ya kaburi hilo akachutama na kusoma kibao kilichowekwa mbele ya kaburi hilo ambacho kilikuwa na jina la marehemu.
“Ndiyo hili hili. Jina lake limeandikwa hapa. Thomas Christopher,” akaniambia.
Ili kujiridhisha nilikwenda mbele ya kaburi hilo nikakisoma hicho kibao. Kweli lilikuwa kaburi la Thomas Christopher kwani jina lake lilikuwa limeandikwa.
Wakati ninalitazama kaburi hilo nilikuwa nikijiambia kimoyomoyo, Thomas amekufa lakini bado anaua watu! Inakuwaje?
“Asante mzee. Nakushukuru sana. Sasa ngoja nikurudishe nyumbani. Kaburi nimeshaliona,” nikamwambia yule mzee.
“Ulitaka kuliona tu?” mzee huyo akaniuliza.
“Ndiyo, nilitaka kuliona tu ili nijue amezikwa wapi.”
“Ni jamaa yako?”
Kwa vile sikutaka kumfafanulia yule mzee ni kitu gani ambacho nilikuwa nakusudia kukifanya na kwa sababu gani, nilimjibu kwa mkato:
“Ndiyo.”
Nikatangulia kuondoka. Mzee akanifuata nyuma.
Tulijipakia kwenye gari tukaondoka.
“Ina maana alipokufa hukuwepo?” mzee akaniuliza wakati ninaendesha gari.
“Sikuwepo hapa Tanga,” nikamjibu.
“Ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa nje ya nchi kidogo.”
“Ulikuwa nje kwa shughuli zako?”
“Ndiyo.”
Sikupenda kumdanganya yule mzee, lakini kazi yetu mara nyingine ilihusisha kusema uongo unapokuwa katika uchunguzi, kwani huwezi kuweka wazi kila kitu.
Nilipomfikisha yule mzee nyumbani kwake nilimshukuru nikaagana naye na kuondoka.
Nilikwenda moja kwa moja ofisini kwa afisa upelelezi wa mkoa nikamueleza hatua niliyokuwa nimefikia katika uchunguzi wangu.
“Baada ya kuliona hilo kaburi umepata wazo gani?” akaniuliza.
“Nimepata wazo la kwenda kulifukua ili tuone kama kweli huyo mtu amekufa na amezikwa pale.”
“Una shaka kwamba anaweza kuwa mtu mwingine?”
“Si tumeshaona kilichobainika kwenye makaburi ya kina Unyeke?”
“Wazo lako ni zuri. Kwa vile kaburi lake haliko mikononi mwa serikali, ninaweza kutoa kibali cha kulifukua, si lazima mahakama.”
“Basi kesho tukalifukue tuone.”
“Sawa.”
Baada ya kuzungumza na afisa upelelezi, nilirudi ofisini kwangu, nikaandika maelezo yangu kwenye jalada la uchunguzi wangu kisha nikatoa simu na kumpigia Hamisa.
“Hamisa, habari ya muda huu?” nikamsalimia mara tu alipopokea simu yangu.
“Nzuri. Unasemaje?”
“Kwanini unaniuliza hivyo, si tunasalimiana Hamisa?”
“Kwani si unajua kwamba niko kazini? Au ndiyo umeanza kuchanganyikiwa?”
Bado Watatu – 42 | Mwanaspoti
