Dar es Salaam. Mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameahidi kushughulikia changamoto kubwa zilizopo Kigamboni na Mbagala za barabara, vivuko, umeme na maji.
Aidha, Dk Nchimbi ameahidi ujenzi wa shule tatu za msingi za mchepuo wa Kiingereza, kumalizia na kuanzisha miradi mipya ya maji pamoja na kukuza utalii wa Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Changamoto hizo ambazo Dk Nchimbi ameahidi kufanyiwa kazi, zimewasilishwa na wagombea ubunge wa chama hicho katika mikutano ya kampeni iliyofanyika leo Jumapili, Septemba 28, 2025, Uwanja wa Mji Mwema, Kigamboni na baadaye mkutano Uwanja wa Maturubahi, ukihusisha majimbo ya Mbagala na Chamanzi.
Tayari Dk Nchimbi ameshazunguka mikoa 14 na leo ukiwa ni wa 15, akisaka kura za mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Septemba 28, 2025.
Mikoa mingine aliyotembelea ni Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera, Rukwa, Katavi, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Ruvuma, Njombe na Iringa.
Akizungumza kwenye mkutano wa Kigamboni, Dk Nchimbi amejibu changamoto zilizowasilishwa na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Haran Sanga huku akieleza yaliyofanyika miaka mitano iliyopita na yatakayokwenda kufanyika iwapo chama hicho kitapatiwa ridhaa ya kuongoza nchi kwa mara nyingine.
Mgombea mwenza huyo amesema miaka mitano iliyopita Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa ya maendeleo sambamba na kulinda heshima ya wanawake kuwa wanaweza.
Ametolea mfano, miaka mitano iliyopita, zahanati zilikuwa 4,838 sasa ziko 7,732. Vituo vya afya vilikuwa 626 sasa 1,276 na hospitali za wilaya za halmashauri zimefikia 293 kutoka 174.
Katika sekta ya elimu, Dk Nchimbi amesema shule za msingi zilikuwa 18,099 sasa zimefikia 28,099, za sekondari zilikuwa 5,124 lakini sasa zimefika 6,488.

Amesema uwezo wa uzalishaji umeme ulikuwa megawati 1,602 sasa zinazalishwa megawati 3,078, maji safi na salama mjini yalikuwa asilimia 84 leo asilimia 90, vijijini yalikuwa asilimia 70 na sasa ni asilimia 80.
“Haya ni baadhi ya mafanikio ya kitaifa na hii ndiyo inatupa ujasiri wa kuja tena mbele yenu kuwaomba mmchague mama Samia kwa kura nyingi na za kishindo,” amesema Dk Nchimbi.
Akijibu changamoto za mgombea ubunge, Dk Nchimbi amesema miaka mitano ijayo wanakwenda kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kibada hadi Mwasonga, ujenzi wa barabara Tungisongani hadi Kimbiji JKT, Kibada hadi Stendi, Mji Mwema-Kimbiji hadi Mpemba Mnazi.
“Uboreshaji wa barabara ndogondogo za mtaa,” amesema Dk Nchimbi huku wananchi na mgombea wao wa ubunge wakishangilia.
Kuhusu vivuko, Dk Nchimbi amesema wamedhamiria kupanua maegesho kwenye kivuko cha Kigamboni: “Matengenezo ya vivuko vyetu vya MV Magogoni na MV Kigamboni yutamalizika haraka.”
“Mbunge ameongelea vivuko ambavyo vinasaidia maisha ya wananchi, vitakuwa vinatengenezwa haraka. Mimi pia familia yangu inaishi Kigamboni, kwa hiyo shida yenu ni shida yangu,” amesema Dk Nchimbi.
Miaka mitano ijayo, Dk Nchimbi amesema: “Eneo la Kigamboni tunakwenda kujenga vituo vipya vya afya sita na kuboresha hospitali ya wilaya.”
Katika elimu, Dk Nchimbi ameahidi CCM itajenga shule za msingi nne, kati ya hizo nne, tatu zitakuwa za mfumo wa Kiingereza kuanzia darasa la kwanza.
“Tumedhamiria kujenga sekondari mpya tano na zote hizi za msingi na sekondari zitakuwa za ghorofa. Tunataka Kigamboni iwe ya kisasa,” amesema Dk Nchimbi.
Ameahidi kwenye shule zilizopo za msingi na sekondari, wataongeza madarasa, ili watoto wasibanane na pia watajenga Veta mpya Kigamboni.
Kuhusu eneo la ardhi, Dk Nchimbi ameahidi CCM itasimamia utoaji wa hati za viwanja na upimaji wa maeneo.
Pia, ametoa wito kwa watu wenye maeneo makubwa ambayo hayajaendelezwa kuyaendeleza ili yasiwe mapori na makazi ya vibaka.
Mgombea mwenza huyo amesema miaka mitano ijayo wanakwenda kujenga viwanda vinavyoendana na mahitaji ya wananchi wa Kigamboni kama vile vya samaki na juisi na itaongeza thamani ya Kigamboni.
Katika eneo la ajira, Dk Nchimbi amesema wanakwenda kutengeneza ajira mpya za sekta rasmi na isiyo rasmi milioni nane, kwa hiyo Watanzania wote wenye haki ya kufanya kazi, CCM inakwenda kuwatengenezea maeneo ya kufanya kazi ili kujiajiri ama kuajiriwa.
Katika mkutano wa Maturubahi, Dk Nchimbi amesema barabara ya mwendokasi ya Mbagala imekamilika na kinachosubiriwa ni mabasi yaanze kufanya kazi.
“Mabasi 155 yameshaingia nchini tayari, kinachofanyika sasa ni kukamilisha mambo ya kiutendaji na yakianza kutumika yatamaliza changamoto ya usafiri,” amesema Dk Nchimbi.
“Nia ya CCM kumaliza changamoto ya foleni Dar es Salaam, lakini tumedhamiria kujenga barabara ya njia sita na nne. Jambo zuri na heshima kwa nchi yetu, barabara za mwendokasi kwa Afrika Mashariki ni Tanzania pekee,” amesema Dk Nchimbi.
Pamoja na hayo, Dk Nchimbi amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeishi kauli ya Rais Samia ya kukusanya kodi bila bughudha na kuitaka kuendelea hivyo hivyo.
“Katika Jimbo la Mbagala, tunakwenda kujenga bandari kavu. Hii itaongeza ajira, biashara ya usafiri itaongezeka na kuchochea ajira kwa vijana wetu, kwa hiyo Mbagala inakwenda kukua,” amesema.
Eneo la barabara iliyowasilishwa na mgombea ubunge Kakulu, Dk Nchimbi amesema wamedhamiria upanuzi wa barabara ya Mbagala hadi Kongowe kuwa ya njia nne na nyingine za ndani.
Umeme, barabara na vivuko
Mgombea ubunge wa Kigamboni, Haran Sanga amesema wamejiandaa kuhakikisha ushindi wa kishindo kwake, mgombea urais (Samia) na madiwani.
Amesema Kigamboni ina wakazi zaidi ya laki tatu na waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura ni zaidi ya laki mbili.
Sanga amesema zaidi ya Sh300 bilioni zilipokelewa katika kipindi cha miaka mitano iliyopika ambayo imetumika kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo afya, elimu, miundombinu ya barabara na maji.
Akizungumzia kero ya kivuko, mgombea ubunge huyo amesema; “Kivuko kutoka Feri kwenda Kigamboni ni changamoto nyingine kwa wananchi, lakini vivuko vilivyokuwepo vimekwenda kwenye matengenezo sasa ni zaidi ya miaka miwili, tunaomba mgombea mwenza utusaidie katika hili ili kumaliza changamoto ya wananchi wanayokutana nayo saizi.”
Mkazi wa Kigamboni Kisiwani, Omary Thabiti amesema; “Mimi ni dereva, naendesha gari za Kigamboni- Cheka, barabara inaharibika sana kipindi cha mvua, wanaweza kuziba viraba lakini mvua ikinyesha hali inarudi vilevile. Kwa hiyo, alichokisema mgombea wetu ni sahihi kabisa.
“Lakini Kigamboni hatuelewi stendi ni ipi, kwa hiyo Kigamboni barabara ni changamoto kubwa.”
Mkazi wa Dege, Sunday Sebastian amesema umeme unasumbua, akitoa mfano kwamba unaweza kwenda hospitali ukakosa huduma kutokana na ukosefu wa umeme.
“Mtu unatoka Cheka kufika Hospitali ya Wilaya ni kama kilomita 15, sasa ikifika unaambiwa umeme umekatika na una mgonjwa, sasa mgonjwa anasubiri umeme? Kwa changamoto hii inapaswa itatuliwe ili kwenda sawia na miundombinu iliyopo,” amesema Sebastian.
Mkazi wa Mji Mwema, Suzan Anthony amesema, mgombea ubunge amewasiliasha kero sahihi za wananchi na wanaomba changamoto hizo zitafutiwe ufumbuzi.
“Nampongeza mgombea wetu, ameongea changamoto zetu, hiyo ya barabara, umeme, vivuko na lingine ni migogoro ya ardhi, kwa kweli amepiga mule mule. Naiomba CCM iyafanyie kazi na yakifanyiwa kazi Kigamboni itakuwa vizuri,” amesema Suzana.
Katibu wa Oganizesheni, Issa Gavu Ussi amesema wao kama chama tawala hawaendi kwa wananchi kulalamika na au kunung’unika bali wanakwenda kupeleka sera na Ilani nzuri zenye manufaa kwa Watanzania na taifa kwa ujumla.
“Yapo baadhi ya maeneo ya Kigamboni yenye matatizo ya ardhi, ilani yetu inaeleza na kuelekeza uwepo wa utaratibu mzuri wa wananchi kumiliki ardhi ya kilimo, biashara au makazi.
“Tunategemea mkitupa ridhaa tena, tutatengeneza sera nzuri za kuwafanya wananchi mmiliki ardhi na iwasaidie kwa mipango yenu,” amesema Gavu.
Gavu amewaeleza wana Kigamboni kwamba hakuna chama kingine chenye sera nzuri za kuipeleka mbele Tanzania zaidi ya Chama cha Mapinduzi, hivyo kuwaomba wananchi Oktoba 29, wampe kura nyingi Samia, wabunge na madiwani wa CCM.
Gavu amesema ili kushinda kwa kura nyingi ni lazima wana CCM wahamasishane kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kwenda kupiga kura.
“Tunajua tumefanya mengi kwenye huduma za jamii na ahadi yetu mkitupa ridhaa ni kuongeza kasi ya kuwatumikia, lakini tunawaomba tuendeleze amani, umoja na upendo,” amesema Gavu.

Naye Mbunge wa zamani wa Busega, Mkoa wa Simiyu, Dk Raphael Chegeni amesema katika miaka minne na nusu ya utawala wa Rais Samia, nchi imetulia.
“Mgombea wetu wa urais anachapa maendeleo kila mmoja anayaona. Wanawake hoyeeee….wanawake ni jeshi kubwa. Utulivu hadi kwenye familia ameleta. Sasa Oktoba twendeni tukatiki kwa mama Samia, wabunge na madiwani wa CCM,” amesema Dk Chegeni.
Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amesema bei ya pamba, korosho na kahawa zimepanda na hii ni kwa sababu ya uongozi bora wa Samia.
“Anahangaika na nishati safi, kumtua mama ndoo kichwani, anahangaika na matatizo ya watu na CCM ni chama pekee chenye mipango na mikakati ya kuipeleka nchi mbele. Hao wengine hawana cha kuonesha, tuendelee kuiamini CCM,” amesema Mchungaji Msigwa.
Mgombea ubunge wa Mbagala, Kakulu Burchard amesema utekelezaji wa miradi ya DMDP inaendelea maeneo mbalimbali na makandarasi wapo maeneo ya utekelezaji.
“Maeneo mbalimbali kulikuwa na changamoto ya barabara, lakini ukweli ni kwamba kila mmoja anaona wakandarasi wako ‘site’ na Serikali ya CCM inazitafutia ufumbuzi,” amesema Kalulu.
Kalulu amesema miradi maji na afya imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa jimboni humo.
Mgombea ubunge wa Chamanzi, Abdallah Chaurembo ambaye awali alikuwa mbunge wa Mbagala kabla ya jimbo hilo kugawanywa na kuzaliwa la Chamanzi, amesema zaidi ya Sh180 bilioni zilipokelewa Mbagala na Temeke.
Chaurembo amesema kero yetu kubwa ya barabara ya Rangi Tatu- Charambe hadi Msongola imewekwa kwenye ilani, kikubwa wananchi wamchague Samia ili barabara hiyo ikatekelezwe.
Hakuna wa kuzuia kupiga kura
Kwa upande wake, Mratibu wa kampeni za chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, Richard Kasesela amesema kifungu cha 21 cha Katiba kinampa haki mtu kwenda kupiga kura na kinamzuia mtu kwenda kupiga kura.
“Niwaombe wana Mbagala, Oktoba 29 jitokezeni kwenda kupiga kura, hakuna atakayewazuia kwenda kupiga kura. Mama Samia amefanya makubwa tukampe mitano,” amesema.