Chaumma: Tutafuta njaa, tutarudisha tabasamu la Watanzania

Tanga. Mgombea mwenza wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja, ameahidi kurejesha furaha ya Watanzania baada ya kuingia madarakani.

Minja amesema kukosekana kwa furaha kunatokana na ugumu wa maisha waliyonayo Watanzania, ikiwemo kupanda kwa bei ya chakula, kodi, ushuru, ukosefu wa ajira pamoja na njaa.

Amesema haiwezekani watu wakune vichwa kuhusu kile watakachokula badala ya kuwaza kujenga na kufanya maendeleo, hali inayowafanya kuwa na utitiri wa mawazo na kujikuta wakikosa furaha.

Devotha ametoa kauli hiyo leo, Septemba 28, 2025, mkoani Tanga wakati akiendelea na kampeni za kutafuta kura kuelekea uchaguzi mkuu, ambapo awali alianzia Kata ya Nkumba, Muheza kisha Jimbo la Kilindi.

“Watu hawana furaha kwa sababu wana njaa, kodi zinawasubiri, barabara hazina lami, hawana maji kama hapa Kilindi. Baba akiamka asubuhi anawaza familia yake itakula nini. Hivi mtu wa hivi anaweza akawaza hata kujenga kweli?” amehoji Minja.

Kutokana na hayo, Devotha amesema watu hawana furaha kutokana na maisha wanayoishi ambayo ni magumu, hivyo Serikali ya Chaumma itarejesha furaha punde ikiingia madarakani.

“Tutaondoa kodi kwenye vifaa vya ujenzi, kusamehe kodi kwa wafanyabiashara wanaoanza. Lengo letu ni kurejesha tabasamu kwa watu,” amesema.

Amesema hayo yote yanawezekana kwa kuking’oa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani kupitia kura za Oktoba 29, 2025.

“Tutarasimisha sekta ya maji, watu wapate mtandao wa maji. Tutawapatia rasilimali, ardhi, viatilifu, pembejeo na dawa ili walime, wapate chakula na biashara,” amesema.

Pia, amesema Chaumma kitahakikisha Watanzania wanapata ajira hasa kupitia kilimo, hivyo hawatakuwa na njaa tena, huku akibainisha kuwa njaa inasababisha watu washindwe kufanya kazi na hata kuugua.

Akifafanua zaidi, amesema Chaumma kikiingia madarakani furaha itapatikana kupitia ajira, chakula, barabara za lami na maji.

Mgombea mwenza huyo amesema rasilimali zote ilizonazo Tanzania, ikiwemo bahari, mito, milima na madini, zinapaswa kuwanufaisha wananchi.

Amesema hakutakuwa na kodi ndogo ndogo kwa Watanzania kwani kodi kubwa zitakusanywa katika miradi na sekta zinazoingiza mapato makubwa.

Akitolea mfano Mkoa wa Tanga, amesema: “Tanga ilikuwa na uchumi mkubwa, ilitambulika kwa sifa ya mkonge na viwanda. Tupeni Chaumma turejeshe heshima ya Tanga.”

Amesema uwezekano wa mchele kuuzwa Sh500 kutoka Sh3,000 ya sasa upo, endapo kilimo kitatiliwa mkazo na viatilifu, pembejeo pamoja na dawa kupatikana kwa urahisi.

Akizungumza katika Kata ya Mafisa, Jimbo la Kilindi mkoani Tanga, Devotha amesema Kilindi itabadilika na kuwa jimbo lenye maendeleo endapo wananchi watamchagua mgombea ubunge Rachel Mkadala wa chama hicho.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Kilindi, Rachel Mkadala, amesema atasimamia mapato kuhakikisha maendeleo yanapatikana Kilindi, hususan barabara, elimu, maji na afya.

“Kilindi itapata maendeleo. Zitapatikana barabara za lami, maji na tutatatua migogoro inayoikabili Kilindi kati ya wakulima na wafugaji,” ameahidi Rachel.