Tanga. Jeshi la Polisi limewataka wasichana kuepuka kujipiga picha za utupu na kuzihifadhi kwenye simu za mikononi ili kuepuka madhila na udhalilishaji unaoweza kutokea endapo picha hizo zitasambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
Limesema hata kama mmiliki wa simu hajasambaza picha hizo binafsi, iwapo simu itapotea, kuharibika au kuchukuliwa na mtu mwingine, anaweza kutumia nafasi hiyo kumkomoa kwa kuzisambaza.
Tahadhari hiyo imetolewa leo Jumapili, Septemba 28, 2025, wakati wa mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Al Kheir Girls Seminary, jijini Tanga.
Ofisa wa Dawati la kutoa elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, Happy Milanzi, amesema wasichana wengi hujikuta wakikumbwa na matatizo makubwa, ikiwamo kujiua, baada ya picha zao kusambaa mitandaoni na chanzo chake mara nyingi huwa matumizi mabaya ya simu.
“Nawashauri wanafunzi mnaohitimu kidato cha nne, mkirejea nyumbani msijiingize katika matumizi mabaya ya simu za mikononi. Simu ni kama bomu, likiripuka utaona dunia ni mbaya. Ikiwa utatumia simu, hakikisha ni kwa masuala ya kimaendeleo na masomo,” amesema Milanzi.
Kwa upande wake, Tabia Manjonjo kutoka Dawati la kupinga ukatili wa kijinsia Wilaya ya Tanga, amesema wanafunzi ni miongoni mwa makundi hatarishi kwa kuwa wengi hujikuta wakiiga mienendo ya mitaani.
“Nawasihi wahitimu, msikubali kutumbukia kwenye matumizi mabaya ya simu. Badala yake fanyieni kazi yale mliyofundishwa na kulelewa shuleni, kwa sababu huko mitaani vijana wanawasubiri na msemao wao maarufu ni ‘matoleo mapya yanakuja’,” amesema Tabia.
Mkuu wa shule hiyo, Sheha Mohamed Sheha, amesema jumla ya wanafunzi 55 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, licha ya kuimarika kwenye masomo ya sayansi, pia wamepewa malezi bora yatakayowafanya kuwa mfano wa kuigwa.
“Al Kheir ni miongoni mwa shule zinazofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne na sita nchini. Tumeendelea kupokea taarifa kutoka vyuo vikuu na sehemu za kazi kwamba wanafunzi wetu ni kielelezo cha tabia njema na malezi bora,” amesema Sheha.
Katika risala ya wanafunzi hao iliyosomwa na Mwamvita Khatib na Sheha Ibrahim kwa niaba ya wahitimu, wameomba kusaidiwa kwa wale watakaofaulu lakini hawana uwezo wa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na elimu ya juu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Direct Aid Mkoa wa Tanga, Sheikh Farhat, ameahidi kufanya ukarabati mkubwa wa shule hiyo na kuongeza idadi ya wanafunzi watakaopata ufadhili wa masomo kwa ngazi ya kidato cha sita na vyuo vikuu.