ALIYEKUWA kocha wa viungo wa Yanga, Taibi Lagrouni amejiunga na kikosi cha Olympique de Safi cha Morocco baada ya mtaalamu huyo kuondoka kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 kutokana na mkataba wake kumalizika.
Lagrouni alijiunga na Yanga Julai 18, 2023 na kukitumikia kikosi hicho kwa mkataba wa miaka miwili, ambapo mtaalamu huyo alitua nchini kufanya kazi na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi anayeifundisha kwa sasa Singida Black Stars.
Kocha huyo wa viungo alijiunga na Yanga akichukua nafasi ya Helmy Gueldich, ambaye amefanya kazi kwa ukaribu na Nasreddine Nabi, akiitumikia timu hiyo ya mitaa ya Twiga na Jangwani kuanzia Aprili 20, 2021, hadi Agosti 10, 2023.
Licha ya kuitumikia Yanga kwa msimu wa 2023-2024, pia Lagrouni amewahi kufanya kazi katika timu mbalimbali zikiwemo Ittihad Riadi Fkih Ben Salah, Olympique Khouribga, Chabab Atlas Khenifra na Hassania d’Agadir zote za kwao Morocco.

Katika Ligi Kuu ya Morocco ‘Batola Pro’ msimu huu wa 2025-2026, Olympique de Safi, iko nafasi ya nane katika msimamo na pointi zake mbili, baada ya kucheza mechi mbili na kutoka sare yote, huku ikifunga mabao mawili na kuruhusu pia mawili.
Katika ligi hiyo, RS Berkane ndiyo inayoongoza na pointi sita baada ya kushinda mechi zote mbili ilizocheza hadi sasa, ikiwa sawa na Maghreb Fez yenye pointi sita pia, ikiwa nafasi ya pili, ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Akiwa na Yanga, msimu uliopita, Lagrouni aliweka rekodi tamu na kikosi hicho baada ya kubeba mataji matano, yakiwemo ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA), Ngao ya Jamii, Kombe la Mapinduzi na Yoyota iliyolibeba huko Afrika ya Kusini.