Kriketi T20: Yadav ang’ara Tanzania ikiifunga Botswana

KIJANA mdogo wa Kitanzania, Arun Yadav ndiye aliyekuwa nyota wa mchezo wakati Tanzania ikianza vyema michuano ya kufuzu Kombe la Dunia kwa Kriketi ya mizunguko 20 (T20) kwa ushindi wa wiketi 7 dhidi ya Botswana mjini Harare, Zimbabwe mwishoni mwa juma.

Kwa ujasiri mkubwa, kijana Yadav alitengeneza mikimbio 62 kutokana na mipira 32 na kuipelekea Tanzania kupata ushindi mnene wa wiketi 7.

Botswana ndio walianza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 122 baada ya wote 10 kutolewa na warushaji (bowlers) wa Tanzania.

Kwa utulivu kabisa, Tanzania waliweza kuifukuzia mikimbio 122 kwa kutengeneza mikimbio 123 huku wakipoteza wiketi 3 na hivyo kuandika ushindi wa wiketi 7.

Ushindi huo uliipa Tanzania uongozi wa Kundi B ambalo linajumuisha pia nchi za Zimbabwe na Uganda.

Yadav alishirikiana vyema mkongwe Abhik Patwa ambaye alitengeneza mikimbio 20 kutokana na mipira 9 wakati kina Ally Kimote na chipukizi Laksh Bakrania wakifanya kazi nzuri kwenye urushaji.

Tanzania itakutana na Uganda katika mechi yake ya pili kabla ya kumaliza hatua za makundi kwa kuwakabili wenyeji Zimbabbwe.