Matibabu ya fistula yalivyobadili maisha ya wanawake 207 Lindi

Lindi. Wanawake 207 waliokuwa wakisumbuliwa na fistula ya uzazi na matatizo mengine ya afya ya uzazi, wamerudishiwa heshima, afya na matumaoni ya maisha bora baada ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sokoine mkoani Lindi.

Wanawake hao wamepatiwa matibabu hayo bila malipo kwa takriban miaka mitano, kuanzia mwaka 2019 kwa ushirikiano na hospitali ya CCBRT pamoja na Equinor Tanzania.

Meneja wa Miradi kutoka CCBRT, Yohana Kasawala, akizungumza jana Septemba 27, 2025 amesema kuanzia Septemba 22 hadi 26 waliendesha kambi ya matibabu ya bila malipo kwa wanawake 12 wenye changamoto hiyo mkoani Lindi na maeeno jirani.

“Kambi hii ilikuwa ya mwisho na inakamilisha utekelezaji wa mradi wa matibabu ya fistula mkoani Lindi kati ya CCBRT, Sokoine na Equionor ulioanza mwaka 2019.

 “Mradi huu umetelekezwa kwa mafanikio makubwa kwa zaidi ya asilimia 90, lakini mahitaji bado ni makubwa. Uelewa kuhusu fistula ni mdogo katika maeneo ya vijijini, na wanawake wengi bado wanateseka kimya kimya,” amesema na kuomba wadau wengine waendelee kuwekeza katika huduma hiyo, ili kurejesha utu na thamani ya wanawake wenye changamoto hiyo.

Akizungumzia upatikanaji wa huduma za afya, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sokoine, Dk Alexander Makala, amesema kabla ya mradi huo wanawake waliokuwa na fistula walilazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kutafuta matibabu, jambo ambalo wengi walishindwa kulimudu.

“Wengi waliteseka kimya, wakijificha kutokana na aibu na unyanyapaa. Sasa Serikali kwa kushirikiana na CCBRT na Equinor, tumeboresha huduma hapa Lindi. Tuna wataalamu waliopata mafunzo, vifaa vya kisasa, na huduma bora zinazotolewa kwa wananchi.

 “Tunaomba Serikali yetu, CCBRT na wadau wengine wa sekta binafsi kuendelea kushirikiana katika juhudi hii muhimu kwani tatizo bado halijaisha. Ufadhili zaidi unahitajika ili kuongeza uelewa, kuwezesha uchunguzi wa mapema, na kuhakikisha matibabu bora,” amesema Makala.

Meneja wa Mahusiano ya Jamii wa Equinor Tanzania, Dk Naomi Makota, alitembelea kambi ya upasuaji wa fistula iliyomalizika hivi karibuni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sokoine, amesema wanafurahi kuwa sehemu ya safari ya uponyaji kwa wanawake hao.

“Tunajisikia kuheshimiwa sana kwa kuwa tumekuwa sehemu ya safari hii ya uponyaji pamoja na wanawake hawa jasiri. Dhamira ya Equinor daima imekuwa ni kuwawezesha wananchi si kwa nishati pekee, bali kwa heshima, afya, na fursa. Kuona maisha yakibadilika kupitia huduma ya matibabu na uwezeshaji kiuchumi kunatukumbusha kwanini ushirikishwaji wa jamii unapaswa kuwa kiini cha maendeleo,” amesema.

Saada Hassan (50), mkazi wa Wilaya ya Liwale amabaye ni miongoni mwa wanawake waliopata matibabu, amesema aliishi na fistula kwa karibu miaka 10, huku akipewa majina mabaya na kutokana na hali yake.

Ofisa Mahusiano ya Jamii wa Equinor Tanzania, Dk Naomi Makota akifurahia moja ya mikoba iliyotengenezwa na Rehema Elias aliyewahi kuwa mgonjwa wa fistula na mnufaika wa mafunzo ya ujasiriamali kupitia kituo cha mafunzo cha Mabinti CCBRT yanayofadhiliwa na kampuni hiyo walipomtembelea nyumbani kwake Kijiji cha Mnyambe, halmashuri ya wilaya Mtama mkoani Lindi



“…Nilitengwa na jamii, niliposikia tangazo la redio kuhusu matibabu, nilipiga simu na nikatumiwa nauli. Nilipofika hapa Sokoine, nilipokelewa kwa upendo. Sasa nimepata matibabu na nitarudi nyumbani nikiwa na heshima yangu imerejea,” amesema Saada.

Mwingine ni Amina Juma (si jina halisi), aliyefanyiwa upasuaji mwaka 2021 na sasa anaendesha biashara ya ushonaji huko Nachingwea amesema, “Baada ya matibabu, nilipelekwa Kituo cha Mabinti cha CCBRT. Nilijifunza kushona, kufuma na kutengeneza vitambaa. Leo hii, najitegemea kiuchumi na nawafundisha wanawake wengine.”

Kupitia ufadhili huo, wanawake 33 wamepatiwa mafunzo katika fani mbalimbali kama ushonaji, utengenezaji wa mikufu, na kuchomelea kwa sindano.

Kasawala amesema kila muhitimu hupatiwa kifurushi cha kuanzia, ikiwemo mashine ya kushonea, vitambaa, na vifaa vingine ili waanze maisha mapya ya kujitegemea.

“Wanawake hawa hufika hospitali ya CCBRT wakiwa wamejeruhiwa kimwili na kisaikolojia, lakini kupitia upasuaji, huduma za utengamao na mafunzo ya ujasiriamali hupona kabisa na kuanza kujitegemea,” amesema.