Mbinu za kutatua migogoro kwenye ndoa

Uhusiano wa watu wengi umefikia katika hali mbaya na mwingine kufa kabisa, huku wanandoa wakiachana katika maumivu na majeraha makali ya moyo.

Chanzo kikubwa kikiwa kutojua kwao kuishughulikia migogoro inayojitokeza katika uhusiano wao.

Mara nyingi katika ushauri tunasema shida sio kujikuta ndani ya migogoro bali shida ni namna mnavyoishughulikia migogoro hiyo.

Unapoona uhusiano wa wengine ni mzuri na wa kutamanisha, haimaanishi nao hawana migogoro, bali wanao lakini tofauti ni ujuzi wao wa kushughulika na migogoro hiyo.

Kiu yangu ni kwamba, mwisho wa kusoma andiko hili ufahamu namna ya kuboresha uhusiano wako kupitia kujua jinsi bora za kushughulikia migogoro baina yako na mke au mume wako pamoja na wote wanaokuzunguka.

Tunaziona ndoa na uhusiano vikiwa na maumivu, machungu na mapigano kuliko nyakati za amani na maelewano.

Wale walioweza kuimarisha amani na maelewano katika uhusiano wao sio kwamba ni pacha na wanafanana katika kufikiri na kutenda kwao, sio kwamba wameumbwa wenye tabia za kufanana na mtazamo sawa, bali ni wale waliojifunza kuchukuliana na tofauti zao, wakizikubali na kuzielewa vema na kila mmoja akijaribu kuujazia udhaifu wa mwenzake.

Wamejifunza kuzungumza kila mmoja kwa lugha ya mwenzake wakizielewa haiba zao na kubadilika kutokana na hali halisi.

Kwakuwa wote hatufanani, na tofauti hizi tunaingia nazo katika uhusiano wetu, daima lazima tofauti ziibuke baina yetu, na sio kwamba mgogoro huwa mmoja bali huwa mingi, midogo na mikubwa, na wala hili sio jambo baya na la kushangaza, bali ni kitu cha kawaida.

Nini maana ya mgogoro? Ni kutofautiana baina ya watu, kupingana, kutoafikiana katika jambo fulani au mawazo fulani. Hapa naangalia zaidi migogoro inayotokea katika muktadha wa ndoa.

Kati ya njia za kizamani ambazo zinatumika na wanandoa wengine katika kushughulikia migogoro ni kuinyamazisha, kuifukia na kujitahidi kuisahau migogoro hiyo.

Njia hii imetumika sana hasa kwa wale wanaoshika dini zao. Kwa kuzika na kufunika migogoro hatutatui bali tunajenga na kukomaza maumivu ya ndani na chuki ambayo taratibu inabadilisha mitazamo yetu kuwa mibaya kwa wale tunaowapenda.

Kumbuka, tofauti hizi zinapozikwa, huzikwa zikiwa hai, na hivyo lazima zitafufuka na kuleta shida.

Wanandoa wengine hushughulikia migogoro yao kwa kuamua kupakua kila kilichopo moyoni na kukimwaga kwa aliyewaudhi.

Tumesikia wengi wakisema “mpe vidonge vyake”, “mpakulie” kwa wengine njia hii imezaa vita na magomvi tele. Neno baada ya neno, jibizano baada ya jibizano na hatimaye kofi na ngumi navyo vikaingia kazini.

Kutokana na tafiti tulizozifanya kwa wanandoa wengi na wale wengine walio katika uhusiano, wengi wameelezea kuumizwa sana na viugomvi vya mara kwa mara vinavyosababishwa na mgogoro fulani baina yao. Kumbuka kuwa migogoro inaweza kushughulikiwa pasipo ugomvi.

Ugomvi maana yake ni vita ya maneno ambayo inaruhusu hisia za hasira kuchukua nafasi, na hapa wanandoa hawaangalii tena sababu za mgogoro wao bali wanaanza kulengana wenyewe binafsi na kushushiana maneno, matusi na lawama.

Maandiko yanasema “Wapumbavu hugombana wakati wote bali wanaoepusha magomvi huleta heshima”.

Katika kushughulikia migogoro inakupasa uyafahamu migogoro ni jambo asilia na kwahiyo haliepukiki.

Kama nilivyokwisha kusema awali kwamba wote sisi tumetokea katika tofauti, mitazamo yetu na matakwa yetu ni tofauti na kwahiyo tutegemee kabisa kutofautiana katika chaguzi zetu, mapendeleo yetu, mitazamo yetu nk. Migogoro pia haiepukiki hususani kwa watu wanaopendana na wenye kiu ya kudumisha pendo lao zaidi. Migogoro ya mara kwa mara baina ya wanandoa ni ile ya maneno, hii kwa jinsi ilivyo peke yake haidhuru kitu, kwa kugemea na kupevuka kwa wale waliotofautiana. Wako wanaoweza kutofautiana, wakalumbana kwa maneno na wakaishia mwisho mwema, wako wanaolumbana na kuishia katika kupigana.

Migogoro huonyesha kunyimwa au kudhulumiwa kwa hadhi au hitaji la mmoja baina ya wanandoa

Kila mtu ana mahitaji binafsi na ya msingi katika uhusiano. Mtafiti William Glaser anasema kati ya mahitaji ya msingi ya mwanadamu ni hitaji la kupenda na kupendwa na hitaji la kujiona au kuonwa wa thamani na unayefaa na unayestahili. Mara unapoingia katika mgogoro na mke au mume wako, jiulize, ni hitaji gani ambalo halijatimizwa? Maana kwa kutokutimizwa kwa hitaji lolote lako, lazima itasababisha mgogoro kunyanyuka.