Mbeya. Mgombea ubunge wa Mbarali, Bahati Ndingo, amewaomba wananchi kumpa ridhaa kwa kipindi kingine ili akatatue changamoto ya ubovu wa barabara, huduma ya maji safi na nishati ya umeme vijijini.
Amesema huduma hizo zitachochea kukua kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi, hususan wakulima wa zao la mpunga, kusafirisha kutoka mashambani kwenda sokoni.
Ndingo amesema hayo leo, Septemba 28, 2025, kwenye mkutano wa kampeni, akinadi ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025-2030 sambamba na kuomba kura za mgombea urais, Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine, Ndingo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, kama sehemu ya kutekeleza takwa la kisheria na kutimiza wajibu wao.
Amesema anatambua changamoto za ubovu wa barabara, huduma ya maji safi na nishati ya umeme, jambo atakaloanza kutekeleza na tayari lipo kwenye utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya miaka mitano ijayo.
“Nimetoa ahadi, nina uhakika tayari zipo katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2025/30, lakini pia ilani iliyopita Serikali imetekeleza katika nyanja mbalimbali za elimu, afya na nyinginezo,” amesema.
Ndingo amesema akipata ridhaa atapelekea maendeleo ya haraka Jimbo la Mbarali sambamba na kuanza na vipaumbele vya barabara, maji safi na nishati vijijini.
“Wana Mbarali, nimekuja tena kwenu kuomba ridhaa, lakini pia naomba jitokezeni kwenye uchaguzi Oktoba 29, 2025, kupiga kura za kishindo za mgombea urais, Samia Suluhu Hassan,” amesema.