Milima, mabonde kampeni za uchaguzi zikifikisha mwezi mmoja

Dar es Salaam. Kampeni za vyama vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, zimetimiza mwezi mmoja sasa tangu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilipotangaza rasmi kuanza kwa kampeni hizo, Agosti 28, 2025.

Vyama hivyo vilianza kufanya kampeni zao kwa kuwanadi wagombea wao wa urais, ubunge na udiwani sambamba na kunadi ilani za vyama vyao huku wakiahidi mambo mengine watakayoyafanya katika miaka mitano ijayo.

Katika kipindi hicho cha mwezi mmoja, wagombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan na yule wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ndiyo wameonekana kutembea sehemu kubwa ya nchi wakiomba kura.

Samia na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi wamezunguka katika maeneo tofauti wakiomba kura kwa wananchi huku mikutano yao ikifurika maelfu ya watu wanaokwenda kusikiliza ahadi za chama hicho tawala.


Vilevile, Mwalimu pamoja na mgombea mwenza wake, Devotha Minja wanazunguka kona tofauti za nchi wakinadi ilani ya chama chao na kuahidi mambo watakayoyafanya wakipewa ridhaa na wananchi.

Wakati vyama hivyo vikichanja mbuga, wagombea wa vyama vingine pia wamekuwa wakifuatia kwa mbali wakifanya mikutano ya hadhara katika baadhi ya maeneo. Hata hivyo, baadhi ya vyama vimekuwa vikisuasua huku vikilalamikia ukata kuwa kikwazo kwao.


Mbali na mikutano ya hadhara, kampeni kwa njia ya mabango na kutumia vyombo vya habari imekuwa ikitumiwa zaidi na CCM huku vyama vingine vya upinzani vikieleza kukosa rasilimali fedha za kuwawezesha kuweka mabango kila kona ya nchi.

Ukiwa umebakia mwezi mmoja mwingine, vyama hivyo vina kibarua cha kukamilisha kampeni zao kwa kuhakikisha wanawafikia wananchi katika kona zote ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.

Tofauti na chaguzi zilizopita, mwaka huu vyama vya siasa vimepewa magari ili kuwasaidia katika kampeni zao kwa kuwafikia wananchi kwa urahisi, jambo ambalo limepokewa kwa mitazamo tofauti na viongozi wa vyama hivyo.

Wapo wanaoona magari hayo hayawasaidii kwa sababu wanaingia gharama ya mafuta.

 Wengine wanaona gari moja halitoshi kutumiwa na chama cha siasa. Hata hivyo, wapo wanaosema magari hayo yamewasaidia kuwafikia wananchi.

Kwa upande wa Zanzibar, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilitangaza Septemba 11, 2025 kuwa siku ya kuanza kwa kampeni visiwani humo, hata hivyo baadhi ya vyama bado havijazindua kampeni zao hadi sasa kikiwamo cha NCCR-Mageuzi.

Vingine vilivyozindua kampeni zao, navyo vimetokomea, kampeni zimebaki kwa vyama vya CCM kupitia mgombea wake wa urais, Dk Hussein Mwinyi na mgombea urais kupitia ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman.

Katika kipindi cha mwezi mmoja, ahadi nyingi za wagombea zimetamkwa huku nyingine zikionekana dhahiri kuwa vichekesho na nyingine zikitoa matumaini kwa wananchi endapo watapatiwa ridhaa ya kuongoza Serikali.

Moja ya ahadi kubwa aliyoitoa Samia ni kuanza kwa majaribio ya bima ya afya kwa wote ndani ya siku 100 za kwanza akiwa madarakani.

Pia, ameahidi kuacha kuzuia maiti hospitali, bali wataweka utaratibu kwa ndugu wa marehemu kulipia au kusamehewa kwa wasio na uwezo.

Wakati huohuo, mgombea urais wa Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP) , Kunje Ngombale Mwiru ameahidi endapo atachaguliwa, atajenga bwawa la mamba ikulu na humo watatupiwa mafisadi ili waliwe na mamba hao.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir ametoa ahadi ya kutoa posho ya Sh500,000 kwa kila Mzanzibari kila mwezi, baada ya kula kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar.

Zaidi ya yote, amani na usalama vimetawala katika mikutano ya kampeni katika mwezi huo mzima. Vyama vinapatiwa ulinzi na Jeshi la Polisi, wagombea nao, licha ya kupewa magari na dereva, wanapewa pia na mlinzi.

Vyama vyatathmini kampeni

Wakizungumza na Mwananchi, viongozi wa vyama vya siasa wanasema maandalizi ya mwaka huu na ushirikiano wanaoupata ni wa mfano, jambo linaloonesha mwelekeo wa demokrasia unaoweza kuleta taswira mpya ya kisiasa nchini.

Viongozi hao wanaeleza kuridhishwa kwao na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa wadau mbalimbali wa siasa, wakiwamo wananchi, mamlaka za uchaguzi na vyombo vya habari.

Katibu Mkuu wa AAFP, Rashidi Rai, ambaye chama chake kimejikita zaidi kwenye masuala ya kilimo, anasema hali ya kampeni katika mwezi huu mmoja, imekuwa chanya.

“Kwa upande wetu AAFP, tuko vizuri na tunapata ushirikiano kwa asilimia 100,” anasema kwa ufupi.

Katibu Mkuu wa  Chama cha The United Democratic Party (UDP) na mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Saum Rashid, anasema pamoja na changamoto za kifedha kwa baadhi ya waandishi wa habari waliopo vijijini, kampeni zao zimeendelea vizuri.

“Mimi naona tunaendelea vema sana. Tunapata ushirikiano wa kutosha, changamoto iko wilayani na vijijini, waandishi hawana bajeti,” anasema Saum, akionesha kuridhishwa kwake na mwenendo wa kampeni hizo katika mbio zake kuusaka urais.

Katibu Mkuu wa Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) na mgombea urais wa chama hicho, Hassan Almas, anasisitiza kuwa uchaguzi wa mwaka huu una sura ya pekee, akiuona kama wa kihistoria.

“Sisi NRA, huu ni uchaguzi wa kihistoria, ni uchaguzi wa mfano wa kuigwa. Ni uchaguzi huru na wa haki, tulijiandaa vizuri kwa nafasi hii tunayogombea, tangu tuzindue kampeni Septemba 5 hadi leo tumezunguka mikoa 17 nchini kwa amani na heshima kabisa,” anasema.

Almas pia anaeleza kufurahishwa na namna vyombo vya habari vinavyoshirikiana nao, pamoja na hatua ya wagombea wote kupewa magari mapya ya kampeni hali anayoona ni jambo lisilo la kawaida, hivyo linafaa kuenziwa katika chaguzi zijazo.

“Wagombea wote wa urais tumepewa magari mapya kabisa ziro km. Hili si jambo la kawaida, ni jambo la kupongezwa kabisa. Kuhusu vyombo vya habari mambo ni mazuri sana, kampeni zetu zinarushwa mubashara na vyombo vinaripoti vizuri sana,” anasema.

Kwa upande wa Chama cha United Peoples Democratic (UPDP), mgombea urais wa chama hicho, Twalib Kadege anasema ulinzi na amani vimetawala katika kampeni zake huku akitaka vyombo vya habari kuongeza ufuatiliaji wa wagombea wote.

“Najua ni wajibu wa vyombo vya habari kuamua namna ya kuandika wagombea, mimi kama mgombea siwezi kuvilaumu japo kwa upande wangu sioni tukiandikwa sana hasa kuwekwa kurasa za mbele magazetini, sioni.

“Kuhusu hali ya usawa na mwenendo kwa jumla, uchaguzi unaenda vizuri kabisa tunapatiwa ulinzi wa kutosha na kampeni tunafanya kwa uhuru kabisa,” anasema Kadege.

Msemaji wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Bakari Makame anatoa wito kwa mamlaka za uchaguzi kuona namna ya kuwezesha kampeni za wagombea ubunge kama ilivyo kwa wagombea urais ili wafanye kampeni zao vema


“Mgombea urais analindwa na bodigadi tu, hana ulinzi nyumbani kwake, mwaka huu tunaona tofauti maana kwa kawaida mgombea urais hupewa ulinzi kwenye kampeni zake na nyumbani kwake.

“Wagombea ubunge wapewe fedha wanashindwa kufanya kampeni, uchaguzi umepoa tunakosa ladha ya kampeni tulizozizowea,” anasema Makame ambaye ni msemaji wa chama hicho.

Tathmini hizo kutoka kwa wagombea wa upinzani zinaashiria mwanga mpya katika uwanja wa siasa, huku wadau wakisubiri kuona jinsi kampeni zitakavyoendelea kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.