MSHAMBULIAJI wa AaB Fodbold ya Denmark, Kelvin John licha ya timu yake hiyo kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Lyngby Boldklub amezidi kuwa bora na amesema huu ni msimu wake wa kuonyesha kiwango bora.
Jana, timu ya Mtanzania huyo ilipoteza mabao 2-1 dhidi ya Lyngby Boldklub kwenye muendelezo wa Ligi Daraja la Kwanza Denmark na licha ya kufungwa, John alionyesha kiwango bora kwa kufunga bao moja ambalo linamfanya kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mechi, kura zinazopigwa na mashabiki.
Bao alilofunga linamfanya kufikisha jumla ya mabao sita kwenye mechi 10 alizocheza. Timu hiyo ipo nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi baada ya kukusanya pointi 14.
Akizungumza na AaB TV, John alisema huu ni msimu wake wa kufanya vizuri, kuonyesha kiwango bora na kuwa na muendelezo wa kufunga.
“Ninapofunga kila mechi inanipa ujasiri wa kuendelea kufunga, hivyo huu ni msimu wangu wa kufanya vizuri na kuisaidia timu yangu imalize nafasi nzuri,” alisema John.
Huu ni msimu wa pili kwa John kuitumikia timu hiyo ambayo msimu uliopita ilimaliza mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Denmark na kushushwa daraja, hivyo sasa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Mbali na nyota huyo wa zamani wa Genk ya Ubelgiji, Watanzania wengine wanaocheza mataifa mbalimbali nje ya Afrika wikiendi hii ni Haji Mnoga anayeitumikia Salford City na alimaliza dakika 90 lakini timu hiyo ilipoteza mabao 2-1.
Wengine ni Julietha Singano na Enekia Lunyamila wanaokipiga FC Juarez inayoshiriki Ligi ya Wanawake Mexico juzi walipokea kichapo cha mabao 4-0 huku chama la Aisha Masaka likipoteza kwa mabao 3-1 mbele ya mabingwa watetezi wa Ligi ya Wanawake England Chelsea.