Mtanzania ana kibarua michuano ya Ulaya

CHAMA la Mtanzania, Sabri Kondo anayekipiga BK Hacken ya Sweden, Alhamisi hii watakuwa na kibarua cha kutafuta pointi tatu mbele ya Shelbourne FC ili kutafuta nafasi ya kufuzu michuano ya UEFA Conference League.

Kondo alisajiliwa msimu huu akitokea Coastal Union, alipoitumikia kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea Singida Black Stars.

Chama hilo linatafuta nafasi ya kufuzu mbele ya Shelbourne FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Ireland na ilifika hatua hiyo baada ya kuvuka raundi tatu za awali.

Tangu asajiliwe, alicheza mechi moja ya mtoano ya michuano hiyo mikubwa Ulaya kwa dakika 44, na hadi sasa zikiwa zimechezwa mechi 24 za Ligi Kuu Sweden, kiungo huyo mara kadhaa alianzia benchi na nyingine hakuwepo kikosini.

Akizungumzia ushindani wa namba kikosini, Kondo alisema kila mchezaji anapambana kupata nafasi, hivyo usipofanya jitihada unakosa namba moja kwa moja kikosini.

“Najitahidi kupambana kwa sababu ligi ya Sweden ni kubwa Ulaya, juhudi mazoezini ndiyo zinakupa nafasi ya kucheza na kuna ushindani mkubwa wa namba kwa sababu wachezaji wengi tunaocheza nao wametoka ligi kubwa,” alisema Kondo.

Kondo anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa klabuni hapo baada ya mwaka 2023, Aisha Masaka kusajiliwa kwa upande wa wanawake akitokea Yanga Princess.

Kiungo huyo anaingia kwenye kitabu cha kuwa Mtanzania mwingine kucheza michuano hiyo mikubwa baada ya Mbwana Samatta kucheza akiwa na PAOK ya Ugiriki, Novatus Miroshi akiwa na Shakhtar Donetsk ya Ukraine, na Aisha Masaka alipoitumikia BK Hacken na kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa Wanawake.