MABINGWA wa zamani wa Tanzania, Mtibwa Sugar jioni ya leo imezinduka katika Ligi Kuu msimu huu kwa kuinyoosha Fountain Gate kwa mabao 2-0 na kuzidi kulizamisha jahazi la wapinzani wao hao wanaoburuza mkia ikipoteza mechi zote tatu za awali ilizocheza hadi sasa.
Fountain iliyotoka kuchapika kwa mabao 3-0 mbele ya Simba ilianza msimu wa 2025-2026 kwa kichapo cha bao 1-0 nyumbani ilipoumana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mjini Babati Manyara na leo tena ikiwa ugenini mjini Dodoma ilikubali tena kichapo hicho.
Katika mechi hiyo ambayo ilipigwa katika Uwanja Jamhuri, jijini Dodoma, Mtibwa iliyowahi kubeba ubingwa wa Bara msimu wa 1999 na 2000 ilipata bao la kwanza dakika ya 17 kupitia kwa Andrew Simchimba.
Bao hilo lilidumu hadi mapumziko kabla ya kipindi cha pili wenyeji kuongeza bao la pili dakika ya 48 kutokana na beki wa Fountain Lamela Maneno kujifunga katika harakati za kuokoa hatari.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa Mtibwa iliyorejea Ligi Kuu msimu huu kutoka Ligi ya Championship sambamba na Mbeya City, kwani katika mechi ya awali ilitandikwa 1-0 na Mashujaa mjini Kigoma.
Kipigo hicho kimeifanya Fountain kuwa timu pekee ambayo haijapata hata pointi moja tangu kuanza kwa msimu huu, zikiwa zimeshapigwa mechi 17 hadi sasa na kuifanya isalie mkiani ikizibeba klabu nyingine 15 zinazoshiriki ligi hiyo yenye timu 16 na inayoongozwa na Dodoma Jiji kwa sasa.
Baada ya mechizo timu hizo zitarudi tena uwanjani mara baada ya mapumziko ya wiki mbili kwa ligi hiyo, ambapo Fountain itakuwa nyumbani kubvaana na Dodoma Jiji wakati Mtibwa itaialika Coastal Union kwenye Uwanja wa Jamhuri inayoutumia kama wa nyumbani.