Kuna usemi maarufu kuwa unaweza kuchagua marafiki, mwenza na hata maadui lakini si ndugu. Uwatake, usiwatake, ndugu wapo. Ndugu hatuwatengenezi wala kuwatafuta bali kutengenezewa na wazazi wetu.
Hivyo, ndugu haepukiki katika maisha. Hatuna maana kuwa ndugu hawahitajiki. La hasha! Wanahitajika ila si katika kila jambo. Wanahitajika kwenye msaada na uzuri ili si katika hujuma.
Leo, tutadurusu nafasi ya ndugu katika ndoa. Kama tulivyoonyesha hapo juu, si gharama kuwa na ndugu japo ni gharama kuingia katika na kuitunza ndoa. Hivyo, pamoja na uwepo na umuhimu wa ndugu, tunapaswa kujua kuwa wao si washirika wala wabia katika ndoa kutokana na ukweli kuwa ndoa huingiwa na watu wawili wenye malengo yao binafsi, ingawa yanaweza kuleta faida kwa jamii kama kuzaa na kulea watoto ambao ni mali yao pamoja na jamii na taifa kwa ujumla.
Karibu kila mtu ana ndugu ingawa si kila mtu yuko kwenye ndoa. Na hata walio kwenye ndoa, si wote wanaoifaidi kutokana na sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa ni kutokana na uhusiano mbaya ama baina yao au baina yao na ndugu zao.
Ndugu wanaweza kujenga ndoa na hata kuivunja. Kuna sababu mbalimbali za kufanya hivyo. Wapo wajinga na wenye roho mbaya wasiopenda furaha ya wenzao.
Hawa, si rahisi kufurahi kuona wengine wakifurahi isipokuwa wao. Wengine husukumwa si na husda tu bali hata ujinga.
Sisi kama wanandoa wakongwe, tunamshukuru Mungu. Ndugu zetu si kikwazo katika ndoa yetu. Ndugu zetu si malaika. Ni wanadamu kama wewe na sisi. Kilichofanya ndugu zetu wasiwe kikwazo wala tishio kwa ndoa yetu, ni ile hali ya kuwaonyesha mwanzo na mwisho wa mipaka yetu. Si kwao tu hata sisi kwao, kama wanandoa wenzetu, tuna mipaka yetu. Hatuwatumii tunapotofautisha hasa kuadhibiana au kukomoana.
Je, utajuaje kuwa umevuka mpaka wa ndoa? Tutatoa mifano ya wazi. Kaka yako au mdogo wako ametokea kuoa mke ambaye hakupendi wewe na ndugu zako. Kaka yako anajua.
Wote mnajua lakini ndugu yenu anaonekana kukubaliana na anayofanya mkewe, yaani kuwachukia ndugu wa mumewe. Je, unafanyaje hapa? Badala ya kuhangaishwa nao, unachukua hamsini zako bila kuvunja udugu na nduguyo.
Punguza kumtembelea na hata kumuomba msaada vinginevyo hakuna jinsi. Usimuonyeshe nduguyo kuwa, nawe, kama mkewe, anavyokuchukia au kuwachukia, unamchukia. Hii ni kutokana na ukweli kuwa ndugu yenu alimchagua mwenza wake kwa faida na sababu zake.
Hali hiyo hapo juu huwa rahisi sana kwa wanandoa. Badala ya kuhangaishwa na kwanini mke wa nduguyo hawapendi, pendaneni na kumuachia chuki yake. Maana, ukianza jino kwa jino, utaanza kuwa chanzo cha kuvunjika ndoa kama ndugu yenu atakuruhusu kama ambavyo wewe huwezi kumruhusu ahangaishwe na ndoa yako.
Ndoa ni ya mwenye kuiingia na si mali ya familia ingawa inagusa familia. Hii haina maana kuwa tunaunga mkono wenye tabia mbaya za kimaskini na roho mbaya za kuchukia ndugu wa wenza wao. Hapa, tatizo ni kwamba, mkiwa wote wapumbavu, mtavunjiana ndoa bila sababu.
Ndoa ni kama mali nyingine binafsi. Mfano, duka langu, haliwahusu ndugu yangu isipokuwa mimi na mke au mume wangu.
Hata watoto wetu haliwahusu. Hivyo, kama tusivyojiruhusu mali zetu kuchezewa na wengine au kuingilia na kuchezea zao, tunapaswa hivyo hivyo kuepuka kuingilia ndoa za watu.
Kabla ya kumaliza mada ya leo, tunapaswa tutoe angalizo na tahadhari. Tunapoongelea ndugu, hatuwahusishi wazazi. Hawa, ni kitu kingine kutokana na ukweli kuwa, bila wao, sisi tusingekuwapo.
Isitoshe, ukiwaonea, wana uwezo wa kulaani japo wengi hawaamini katika hili. Jaribu kujikumbusha wengi uwajuao waliowaonea wazazi wa wenza wao. Wengi, kama si wote, huwakuta ya kuwakuta. Wengine huenda mbali na kuonya kuwa, ukimpiga au kumtenza vibaya mzazi wako au wa mwenzio, nawe wanao au wakamwana watawalipia kwa kukutenza vivyo hivyo.
Tumalizie kwa kuonya kuwa ndugu wanaweza kujenga au kuvunja ndoa kama mtawaruhusu au kuwawezesha kufanya hivyo. Kwa wanaowachukia ndugu wa wenza wao, wajue ni tabia ya ovyo na haina faida.