Unguja. Mgombea wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT – Wazalendo, Othman Masoud Othman, maarufu OMO, ameahidi kuyageuza mazao ya bahari kuwa sekta rasmi yenye mchango mkubwa ili kukuza uchumi wa visiwa hivyo.
Othman ameeleza hayo leo Jumapili, Septemba 28, 2025 wakati akizungumza na wavuvi na waanikaji wa dagaa eneo la Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini B, Unguja,
Othman amesema rasilimali za bahari za Zanzibar, ikiwemo mwani na dagaa, zimesalia kuwa wimbo wa kisiasa bila utekelezaji, jambo linalowanyima wananchi wa visiwa hivyo, fursa ya kufaidika moja kwa moja.
“Dagaa ni biashara kubwa sana inayoweza kuingiza kipato kikubwa kwa wananchi wetu na kusaidia kukuza uchumi wa nchi, lakini kutokana na mifumo iliyopo, wageni ndio wanaofadika,”
“Niwaahidi, Serikali nitakayoiunda itageuza sekta hii kuwa rasmi na kuhakikisha dagaa wa Zanzibar wanauzwa katika masoko mbalimbali duniani,” amesema Othman.
Othman ambaye ni mwenyekiti wa ACT – Wazalendo, amesema ni jambo la kusikitisha kuona wafanyabiashara wakiendelea kuanika dagaa chini kwa kutumia mabusati (mikeka) na kutunia nishati ya jua.
“Hii ni dhahiri wakati wa mvua hakuna biashara inayofanyika,” amesema Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Katika hatua nyingine, Othman amesema Serikali ya ACT – Wazalendo itawawezesha wananchi kupitia mikopo nafuu isiyo na vikwazo, ili kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo na wa kati, hususan wale wanaotegemea bahari kama nyenzo kuu ya kipato chao.
Mkazi wa Mangapwani, anayejishughulisha na uanikaji wa dagaa, Makame Issa amesema, “kwa miaka yote niliyofanya shughuli hii, sijawahi kumuona kiongozi wa Serikali au mgombea kufika hapa, ujio wa Othman umetupa faraja kubwa,” amesema.
Kwa upande wake, Maimuna Abdalla amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mazingira wanayofanyiwa kazi kuwa magumu.
“Wakati mwingine tunakata tamaa na kujiona kama si sehemu ya kisiwa hiki, lakini ujio wa mgombea urais wa ACT -Wazalendo, umeleta matumaini mapya kwa wafanyabiashara wa eneo hili,” amesema Maimuna.
Othman anaendelea na mikutano yake ya hadhara ya kunadi sera na vipaumbele vyake utakaofanyika eneo uwanja wa Bumbwini Makoba mkoa wa Kaskazini Unguja jioni ya leo.
Endelea kufuatilia Mwananchi na mitandao yake ya kijamii