PAMBA Jiji jana ikicheza kwa mara ya kwanza mechi y Ligi Kuu Bara ikiwa nyumbani ilibanwa mbavu na Watoza Ushuru wa TRA United baada ya kutoka suluhu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Katika pambano hilo lililokuwa la tatu kwa Pamba na la pili kwa wageni, lilihudhuriwa na mashabiki wachache, huku wenyeji wakishindwa kurudia kile walichokifanya msimu uliopita ilipoizima TRA Utd (enzi ikiifahamika kama Tabora United) kwa bao 1-0 kwenye uwanja huo Aprili 5 mwaka huu.
Ushindi huo wa mechi hiyo ya marudiano ya msimu uliopita ulikuwa ni kisasi kwa Pamba kwani awali ilinyukwa pia bao 1-0 ugenini na Nyuki wa Tabora hao ambao kwa sasa wamenunuliwa na Mamlaka la Mapato Tanzania (TRA).
Pamba Jiji ikitoka kuchapika mabao 3-0 mbele ya watetezi, Yanga katika mechi iliyopita, itajilaumu kwa kushinda kuibuka na ushindi kutokana na kutawala mchezo huo kwa muda mrefu na kuwabana TRA ambayo ilikuwa ikitengeneza mashambulizi ya kushtukia, kupitia pembeni ila ilikosa umakini.
Licha ya makocha wa timu hizo, Francis Baraza wa Pamba na Kassim Otieno kubadilisha baadhi ya wachezaji tofauti na waliotumika mechi zao zilizopita, bado hakukuwa na maajabu kutokana na washambuliaji wa timu zote kukosa utulivu mbele ya lango la mpinzani.
Matokeo hayo ya suluhu imezifanya timu hizo kugawana pointi moja moja, na kila moja sasa kufikisha mbili licha ya kutofautiana idadi ya mechi ilizocheza, zikiwa nafasi ya 13 na 14 mtawalia (hii ni kabla ya mechi ya jioni ya jana kati ya Mtibwa Sugar na Fountain Gate)
Ligi hiyo itaendelea kesho na keshokutwa kabla ya kusimama kwa wiki mbili kupisha mechi za kimataifa kwa timu za taifa na kurejea tena Oktoba 17.