SAID SOUD SAID: Ole wao watakaolalia vitanda vya 6 × 6 Zanzibar

Haina maana kuwa ili ushindane na mtu sharti uwe hukubaliani naye. Inawezekana ukaona anafaa kwa kila nyanja, lakini kwa sababu ushindani umewekwa, unaamua kujitosa kumkabili unayemkubali. Inaitwa ushindani bila chuki.

Said Soud Said ni mgombea urais wa Zanzibar kwenye Uchaguzi Mkuu 2025. Anasema anajitosa kumkabilia Rais aliye madarani, Dk Hussein Ali Mwinyi, lakini wakati huohuo anakubali aina ya uongozi wake, kwamba amefanya vizuri kwenye maendeleo hasa miundombinu, vilevile demokrasia.

Said anasema anaingia kwenye uchaguzi dhidi ya Mwinyi, akiamini kwamba anaweza kumshinda au Mwinyi akashinda. Anaeleza kwamba Mwinyi akishinda itakuwa haki kwa sababu amefanya kazi nzuri inayoeleweka na inayokubalikana kwa Wazanzibari wote.

Msisitizo wa Said ni kuwa anataka apate ridhaa ya Wazanzibari aweze kuwa Rais, shabaha kuu ikiwa kuendeleza maendeleo ambayo yameanzishwa vema na Dk Mwinyi. Ahadi yake ni kuwa atapita alipopita Mwinyi, ila yeye atafanya kwa kasi zaidi.

Said ni Mwenyekiti taifa wa Chama cha Wakulima Tanzania (AFP). Tayari ameshateuliwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuwa mgombea urais wa Zanzibar kwenye Uchaguzi Mkuu 2025. Hivyo, Said ni jina la walio mstari wa mbele kuusaka urais wa Zanzibar na uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Chama chake, AAFP, ndicho kimempa tiketi ya kuusaka urais kwa udi na uvumba. Kwenye Uchaguzi Mkuu 2020, Said pia alisimama kuwa mgombea urais dhidi ya Mwinyi, ambaye wakati huo alikuwa anapambana kusaka muhula wa kwanza.

Kipindi anatangaza kuwania urais Zanzibar mwaka 2020, Said alikuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, aliyekuwa anamaliza muda wake. Nafasi hiyo aliipata kwa kuteuliwa na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, ambaye alikabidhi kijiti kwa Rais wa Mwinyi, Novemba 2020.

Kingine, kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020, Said alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, akiwa ni Waziri Asiye na Wizara Maalumu.

Uteuzi huo, Said aliupata baada ya uchaguzi wa marudio Zanzibar, Machi 20, 2016. Kwa vile chama kikuu cha upinzani Zanzibar wakati huo, CUF kilisusia uchaguzi wa marudio, Shein aliamua kushirikisha vyama vidogo. Said wa AFP (sasa AAFP), alikuwa mmoja wa wanufaika.

Na hiyo imekuwa sababu ya wapinzani ambao hawakuafiki marudio ya uchaguzi Zanzibar, baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, 2015 kufutwa, kuwaita wapinzani walioshiriki marudio Machi 20, 2016 kuwa ni vibaraka. Hata sasa, Said kwa vile alishiriki marudio mwaka 2016 na anamsifu Dk Mwinyi, ananong’onwa kwa mtazamo huohuo.

Said anayajua hayo maneno ya kumuita yeye ni kibaraka. Hata hivyo, anasema wanaomuita kibaraka ni waliofilisika hoja. Anasema, yeye angekuwa mamluki, au anayetumwa, ni kwa nini asingekaa pembeni ili kungoja ateuliwe? Anasema yeye hatumwi, anautaka urais kwa nia ya dhati ili aifanyie Zanzibar mabadiliko anayokusudia.

Hajachipuka ghafla kama uyoga, bali ipo mizizi, shina na matawi, ambayo yanaweza kutoa simulizi ya Said ni nani. Kwanza hii si mara yake ya kwanza kugombea urais Zanzibar. Baada ya kuteuliwa na chama chake cha AAFP kuwa mgombea urais Zanzibar, imekuwa mara ya nne.

AAFP walipomteua Said kuwa mgombea urais Uchaguzi Mkuu 2020, aliahidi kwamba safari hiyo ingekuwa ya mwisho na asingewania tena nafasi hiyo endapo angeshindwa. Hata hivyo, amesaliti ahadi yake na ameingia tena ulingoni 2025.

Mara ya kwanza, Said aligombea urais Zanzibar Uchaguzi Mkuu 2010, kisha alijitosa tena Uchaguzi Mkuu 2015, kisha 2020. Mara zote tatu, aliingia ulingoni kwa tiketi ya AAFP.

Hata mwaka 2010, haikuwa mara ya kwanza kwa Said kugombea nafasi kubwa ya uongozi nchini. Mwaka 2005, Said alishiriki mchakato wa kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa mgombea mwenza wa marehemu Mchungaji Christopher Mtikila, aliyewania urais kupitia Chama cha Democratic (DP).

Said alijiunga na DP mwaka 2003 akitokea Tanzania Labour Party (TLP), alikojiunga mwaka 1996, na aligombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, jimbo la Wawi mwaka 2000 kupitia TLP.

Hivyo, tangu mwaka 2000, jina la Said limekuwa likitokeza kwenye karatasi za wagombea, katika Uchaguzi Mkuu Tanzania, ingawa kwa nafasi tofauti.

Alizaliwa Mei 12, 1949, katika Kijiji cha Kiuyu, Bikirembo, Pemba, akiwa ni mtoto wa tatu, kati ya watano wa familia ya Soud Said Mohamed na Fatma Sheikh Ali.

Kutokana na wazazi wake kutokuwa na uwezo wala fursa ya kumwandikisha shule, ilibidi Said akae bila kusoma mpaka Mapinduzi ya Zanzibar yalipofanikiwa Januari 12, 1964.

Baada ya Mapinduzi Zanzibar, kisha tamko la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Aman Karume la elimu bure kwa kila Mzanzibari, mwaka 1965, Said akiwa na umri wa miaka 16, ndipo alianza darasa la kwanza, Shule ya Msingi Madungu na alihitimu elimu ya msingi mwaka 1972.

Alipomaliza darasa la saba, Said hakupata fursa ya kusoma elimu ya sekondari, badala yake alijikita katika elimu ya dini ya Kiislamu ambako alibobea zaidi.

Na akiwa kijana kabisa, baada tu ya Mapinduzi ya Zanzibar, alijiunga na uliokuwa Umoja wa Vijana wa Chama cha Afro Shiraz (ASP), akawa mjumbe wa vijana wa ASP, jimbo la Wawi, wakati huo ikiitwa Shehia ya Wawi.

Said ni kati ya wanachama wa mwanzo wa Chama cha Mpinduzi (CCM), pale ASP na Tanu (Tanganyika African National Union), vilipoungana Februari 5, 1977.

Kadi yake ya CCM, aliipata Ofisi ya Wilaya ya Chakechake, Pemba. Mwaka 1978, Said alikuwa mjumbe wa kamati ya Mapinduzi (CCM), wilaya ya Chakechake, Pemba.

Mwaka 1992 baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, Said alibaki CCM na alijitolea kushiriki kazi mbalimbali za kukitetea chama dhidi ya vyama vingine. Alishiriki sana harakati chini ya aliyekuwa Waziri Kiongozi Zanzibar, Dk Omar Ali Juma.

Uchaguzi Mkuu 1995, Said alishiriki kampeni mbalimbali za chini kwa chini kuwatafutia ushindi wagombea ubunge, wawakilishi na marais.

Mwaka 1996, alihamia TLP kwa kile alichodai kuwa ndani ya Zanzibar hakukuwa na chama cha upinzani. Akikiita CUF kuwa hakikuwa chama cha siasa cha upinzani, bali chama cha ushindani, kwa vile hakikutaka kupokea matokeo ya kushindwa mwaka 1995. Alijiunga na TLP ili kuonyesha kuwa upinzani wa kweli wa kisiasa ni kukubali kushindwa.

Novemba 3, 2009, Said aliasisi Chama cha Wakulima (AFP, sasa AAFP), kwa kukipatia usajili wa kudumu, kisha akawa mmoja wa wanachama wa mwanzo, pia mwenyekiti wake.

Pamoja na kuwa AAFP, Said haoni aibu wala kosa kuisifu CCM kwamba ni chama cha ukombozi, kwa maana kiliikomboa Tanganyika na Zanzibar na nchi nyingi Afrika, vilevile kimeweza kujipambanua kama chama bora cha siasa.

Anasema, pamoja na sifa hizo, CCM inahitaji kupumzika kwa sababu imeshindwa kuwapa maisha bora wakulima.

Agenda yake nyingine, Said anasema kuwa anataka kuona Wazanzibari wanazaliana na kuongezeka, familia ziwe kubwa. Hayo yatawezekana kwa kuweka sheria kali ya kupiga marufuku vitanda vyenye ukubwa wa futi 6 × 6 (sita kwa sita).

Said anasema kuwa wao enzi zao, hakukuwa na vitanda vya ukubwa wa futi sita kwa sita, ndiyo maana kasi ya kuzaliana ilikuwa kubwa.

Mpango wa Said ni kuhakikisha vitanda vya futi sita kwa sita vinatokomezwa, na endapo atashinda urais, kitanda kikubwa zaidi kwa Mzanzibari kitakuwa futi 4 × 6 (nne kwa sita).