Dar es Salaam. Serikali inatarajia kuongeza idadi ya vituo vya kujazia gesi asilia kutoka 11 vilivyopo sasa jijini Dar es Salaam hadi 18 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupanua upatikanaji wa nishati safi na nafuu kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa kituo cha kwanza cha gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) cha Puma Energy Tanzania kilichopo Tangi Bovu, Barabara ya Bagamoyo.
Amesema Serikali imeondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa vituo vya CNG na vifaa vya mifumo ya gesi kwenye magari ili kuwahamasisha wananchi kuhamia kwenye matumizi ya gesi, ambayo gharama zake ni nafuu ikilinganishwa na mafuta.
Aidha, Mramba amesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeleta magari sita yatakayotoa huduma za kujazia gesi kwa wananchi katika maeneo mbalimbali, huku Puma Energy ikipanga kujenga vituo vingine katika maeneo ya Mandela, Alliance One na Tegeta, ambapo kituo cha Tegeta kinatarajiwa kuwa kikubwa zaidi barani Afrika.
“Kwa niaba ya Serikali, ninatoa wito kwa sekta binafsi na wadau wote wa nishati kuendelea kushirikiana nasi katika kuwekeza kwenye miradi ya gesi asilia na nishati safi. Pia nawahimiza wananchi kutumia fursa hii, kwa kuwa huduma sasa zinapatikana kwa urahisi na gharama nafuu,” amesema.
Kaimu Balozi wa Canada nchini Tanzania, Carol Mundle, amesema mradi wa kituo cha gesi ni uthibitisho wa ushirikiano wa kimataifa.
Amesifu matumizi ya teknolojia iliyotengenezwa Canada na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazokuza miundombinu endelevu na ubunifu nchini.
“Tunajivunia kuona teknolojia ya Canada ikitumika katika mradi huu wa kihistoria. Hii ni taswira halisi ya jinsi ushirikiano wa kimataifa unavyoweza kutoa suluhu ambazo si tu zinachochea ubunifu bali pia zinaunga mkono ajenda ya maendeleo endelevu ya Tanzania,” amesema Mundle.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Puma Energy, Fatma Abdallah, ameeleza maendeleo hayo kama hatua ya mabadiliko kwa Puma Energy na Tanzania.
“Kituo hiki kinachotoa huduma ya vilainishi, gesi na mafuta kinaakisi dhamira yetu ya kutoa suluhu za kisasa na za kuaminika zinazopunguza hewa ya ukaa huku tukiongeza urahisi kwa wateja. Na hii ni mwanzo tu, tunapanga kufungua vituo zaidi vya CNG kabla ya mwisho wa mwaka,” amesema.
Wakati huo huo, imeelezwa kuwa utendaji kazi wa Wizara ya Nishati kupitia taasisi inazozisimamia umezidi kuimarika na kufikia asilimia 96.16 katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2024/2025.
Hayo yamesemwa na Mramba alipofanya kikao kazi cha tano cha tathmini ya utendaji kazi wa Wizara ya Nishati na taasisi zake kwa robo ya nne ya mwaka 2024/2025. Kikao kazi hicho kilifanyika jijini Dodoma mwishoni mwa juma.
Tathmini hiyo iliyofanywa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara ya Nishati imeonesha kuwa katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2024/2025 utendaji kazi wa taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati umeimarika kwa zaidi ya asilimia 96 kutoka asilimia 95 katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025.
Kufuatia tathmini hiyo, Mramba amewapongeza watendaji wa wizara na taasisi zake kwa kuendelea kuboresha utendaji kazi kupitia utekelezaji wa miradi na utoaji huduma kwa wananchi, hali inayoleta matokeo chanya katika sekta ya nishati.
“Tathmini hizi zinaakisi kile tunachokitekeleza, kwani huduma zimeendelea kuboreshwa pamoja na kuimarika zaidi. Sisi kama wizara tumeendelea kuhakikisha kuwa tunatoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Mramba.
Amelipongeza pia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi kwa wakati, jambo ambalo limeleta ongezeko la kuimarika kwa utoaji huduma.
Aidha, kuhusu nishati safi ya kupikia, amesisitiza kutumia mitandao ya kijamii katika kuitangaza nishati hiyo, hususan matumizi ya majiko yanayotumia umeme kidogo, akieleza kuwa mitandao ya kijamii ina nguvu kubwa ya kufikisha habari kwa watu wengi na kwa muda mfupi, lengo likiwa ni kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanahama kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia kwenda kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.