KOCHA wa kikosi cha timu ya taifa ya wasichana U20, Tanzanite Queens, Bakari Shime amesema ingawa timu hiyo imeshinda dhidi ya Angola na kwenda raundi ya tatu ya kuwania fainali za Kombe la Dunia 2026, hajaridhika kwa vile kuna makosa yalifanyika kuanzia eneo la ulinzi na ushambuliaji.
Tanzanite Queens jana ikiwa ugenini ikirudiana na Angola ilishinda mabao 3-0 katika mechi ya kufuzu raundi ya tatu ya Kombe la Dunia mechi iliyopigwa Uwanja wa 22 June na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-0 baada ya awali kushinda 4-0 nyumbani na sasa itakutana na mshindi wa mechi kati ya Kenya na Ethiopia.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, kocha Shime maarufu kama Mchawi Mweusi alisema kwa jinsi walivyocheza, bado kuna kazi ya kufanya hasa katika mechi za raundi ijayo watakapokutana na timu kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki wanaofahamiana wakikutana mara kadhaa.
“Niwapongeze wachezaji walicheza kwa nidhamu kubwa, tulicheza vizuri tulimiliki mpira na kuwanyima nafasi ya kucheza, lakini tumefanya makosa mengi kwenye eneo la ulinzi na ushambuliaji,” alisema Shime na kuongeza;
“Kwa hiyo tunakwenda kufanyia kazi makosa na kurekebisha kwani tukikutana na timu kama Kenya au Ethiopia ambao tunafahamiana tunatoka ukanda mmoja wa Cecafa ni ngumu sana.”
Nahodha wa timu hiyo, Jamila Rajabu alisema wamemaliza kazi Angola na wanarejea Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya mechi za raundi ya tatu.
“Tulifanya kama vile kocha alivyotuelekeza na tumemaliza kazi kwa sasa tunatazama mechi zijazo ili kufanya vizuri na kuandika rekodi kwenye michuano hiyo mikubwa.”
Afrika itawakilishwa na timu nne, Asia (4), Ulaya (6), Oceania (2), Amerika Kaskazini na Kati (4) na Amerika Kusini (4).
Ikifuzu Kombe la Dunia, Tanzanite itakuwa timu ya pili ya taifa ya wanawake kushiriki Fainali za Kombe la Dunia.
Timu ya kwanza ilikuwa timu ya taifa chini ya miaka 17, Serengeti Girls, iliyoshiriki Fainali za Kombe la Dunia na kuishia hatua ya robo fainali mwaka 2022.