TRA Yazindua Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, amezindua Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara litakalosaidia kuwatambua wafanyabiashara ambao hawapo kwenye mfumo rasmi na kutatua changamoto zinazowakabili ili kukuza biashara zao.

Uzinduzi huo umefanyika jana, Septemba 27, 2025, katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, viongozi wa wafanyabiashara na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwenda amesema kuwa baadhi ya wafanyabiashara hukumbana na changamoto za kikodi na mara nyingi hukosa pa kuzipatia ufumbuzi, lakini kupitia dawati hilo changamoto hizo zitasikilizwa na kushughulikiwa.

Amesisitiza kuwa kipaumbele cha TRA ni kuendeleza biashara kwani bila biashara hakuna kodi.

“TRA ni mshirika wa wafanyabiashara. Katika biashara mnazofanya, Serikali pia ina sehemu yake. Badala ya kuwaachia mkabiliane peke yenu na changamoto, tumeamua kushirikiana nanyi kupitia dawati hili. Tunataka kuhakikisha walewajanja wachache wasiibe Serikali na pia wafanyabiashara wa kweli waendelee kufanikiwa,” amesema Mwenda.

Mwenda ameongeza kuwa maono ya kuanzisha dawati hilo yanatokana na ushauri wa wadau na miongozo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa msingi wa maendeleo ya nchi ni kuwezesha biashara.

Aidha, amebainisha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unachangia asilimia 80 ya mapato ya kodi nchini kutokana na wingi wa wafanyabiashara, na kupongeza juhudi zao za kulipa kodi kwa hiari.

Kamishna huyo amefafanua pia kuwa TRA itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara wadogo, akitaja mpango wa kuwajengea machinga soko kubwa litakalowawezesha kufanya biashara kwa ufanisi.

Kuhusu changamoto za kisera, Mwenda alisema Rais Samia tayari ameunda tume ya kupitia mfumo wa kodi na ripoti yake inatarajiwa hivi karibuni. Aliahidi kuwa TRA itashirikiana na tume hiyo kuhakikisha mapendekezo yote yatakayorahisisha biashara yanafanyiwa kazi.

Ameongeza kuwa dawati hilo litashughulikia pia matatizo ya upatikanaji wa mikopo, ucheleweshaji wa mizigo bandarini, ushuru mkubwa, pamoja na gharama kubwa za usafirishaji, hasa kwa wafanyabiashara wa sekta ya logistics.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesema dawati hilo litakuwa nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

“Tunapongeza TRA kwa hatua hii muhimu ya kuwasogezea huduma wafanyabiashara. Dawati hili litawawezesha wafanyabiashara wadogo kukua na kuwa wa kati, na wa kati kuendelea kuwa wakubwa. Hii ni njia ya kuongeza ajira na kipato kwa wananchi,” amesema Mpogolo

Kwa upande wao, wafanyabiashara walilipokea dawati hilo kwa mikono miwili, wakieleza kuwa ni suluhisho la changamoto zao za kila siku.

Mwenyekiti wa Soko la Kariakoo, Severin Mushi, alisema dawati hilo linaenda kutoa majibu ya changamoto nyingi, ikiwemo ucheleweshaji wa mizigo bandarini, ushuru mkubwa, na mzigo wa tozo kwenye miamala ya kifedha.

“Tunataka dawati hili lisiwe la maneno tu bali la vitendo. Tukishirikiana na TRA tunaamini hatutaona tena mizigo ya wafanyabiashara ikipigwa mnada kiholela,” amesema Mushi.

Aidha, alitoa rai kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kulipa Kariakoo hadhi maalumu ya kikodi ili kuvutia zaidi wageni na kukuza “utalii wa kibiashara.”

Dawati hilo linatarajiwa pia kusaidia mageuzi ya mfumo wa malipo kwa kuhamasisha matumizi ya malipo ya kielektroniki badala ya fedha taslimu, hatua ambayo itarahisisha ukusanyaji wa kodi na kuongeza uwazi wa biashara nchini.