Dar es Salaam. Kila kimoja kati ya vyama tisa vya siasa nchini kimetangaza vipaumbele vyake vya utekelezaji ndani ya siku 100 endapo kitapewa ridhaa na wananchi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Miongoni vipaumbele vilivyotajwa na vyama hivyo ni kupatikana kwa Katiba mpya, kudumisha maridhiano ya kitaifa, demokrasia jumuishi, elimu bure kwa ngazi zote na kuendeleza kilimo ili kuinua kipato cha wananchi.
Mbali na hayo, vyama hivyo pia vimeeleza umuhimu wa kulinda uhuru wa kuabudu na kufanya siasa safi, uwekezaji kwenye sekta ya kilimo, upatikanaji wa huduma bora za afya, kupunguza umaskini, kuimarisha uchumi wa wananchi na kutatua changamoto kubwa ya ajira kwa vijana.
Hayo yalielezwa kupitia ilani zao za uchaguzi zilizowasilishwa katika mdahalo uliofanyika leo Jumapili Septemba 28, 2025, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ukiratibiwa na jumuiya ya wanataaluma wa chuo hicho.
Vyama vilivyoshiriki mdahalo huo ni ACT-Wazalendo, Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Chama cha Demokrasia Makini, The United People’s Democratic Party (UPDP), NCCR-Mageuzi, The National League for Democracy (NLD), Democratic Party (DP) na Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA).

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Emanuel Mvula amesema chama hicho kitalenga kuhakikisha haki sawa inapatikana kwa wananchi wote, kuimarisha ustawi wa demokrasia na kukuza uchumi wa kisasa wenye ushindani.
“Baada ya zaidi ya miaka 60 ya uhuru bado umasikini umetanda kwa Watanzania, vituo vya afya havina dawa. Sisi tukifanikiwa kuongoza nchi, tutaweka mfumo wa uwazi serikalini na kuinua uchumi ili uwe wa ushindani zaidi,” amesema Mvula.
Profesa Kitila Mkumbo ambaye ni mgombea ubunge wa Ubungo kupitia CCM, amesema ilani ya chama hicho imeweka kipaumbele kwenye kudumisha demokrasia, kupata Katiba mpya na kupunguza umaskini.
“Tutadumisha demokrasia na utawala bora, tutawezesha upatikanaji wa Katiba mpya na kuongeza ajira kwa vijana. Pia, tutapunguza gharama za maisha na kuboresha mazingira ya wananchi kupata kipato,” amesema Profesa Kitila.
Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma, Bensoa Kigaila amesema iwapo wananchi watawapa ridhaa, ndani ya siku 100 wataunda tume ya upatanishi ili kushughulikia matukio ya utekaji na dhuluma kwa wananchi.
“Tutapeleka bungeni muswada wa Katiba mpya, tutaunda mfumo wa Serikali tatu na pia tume ya ardhi itakayoshughulikia migogoro ya hifadhi inayosababisha vifo kwa wananchi,” amesema.
Mshauri wa Masuala ya Siasa wa DP, Alex Mayunga amesema chama chake kitaweka mkazo katika kulinda afya ya kila Mtanzania na kuhakikisha usalama wa kiuchumi. “Tutahakikisha kila mmoja anaishi katika jamii inayozingatia haki za binadamu,” amesema Mayunga.
Mwakilishi wa NCCR-Mageuzi, Martin Mngongo akizungumza katika mdahalo huo, amesema chama hicho kitajikita kwenye utoaji wa elimu bora, huduma za afya kwa wote na kuhakikisha mazingira huru kwa vyombo vya habari pamoja na asasi za kiraia.
Doyo Hassan ambaye ni mgombe urais NLD, amesema chama hicho kitahakikisha elimu inapatikana bure kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu sambamba na kuongeza fursa za ajira.
“Tutaimarisha demokrasia kwa vyama vya siasa kwa kuwa, hali ya sasa si ya kuridhisha,” amesema.
Mgombea urais kupitia NRA, Almas Hassan amesema chama chake kitadumisha huduma za elimu, afya na kuendeleza mambo mazuri yaliyofanywa na Serikali zilizopita.
Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia Makini Zanzibar, Ameir Hassan Ameir amesema wananchi watasoma bure kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.
“Tutahakikisha kilimo kinakuwa cha kisasa na kila Mtanzania anapatiwa hekari tano za ardhi ili kufanikisha kilimo cha kibiashara,” amesema.
Mgombea urais wa UPDP, Twalib Kadege amesema chama chake kitaweka kipaumbele katika kulinda uhuru wa kuabudu na kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi bila mashinikizo.
Hata hivyo, baada ya kunadi ilani hizo, Profesa George Kahangwa aliwauliza washiriki namna watakavyotekeleza ahadi zao katika mazingira yenye ukosefu wa mwafaka wa kitaifa.
Akijibu swali hilo, mwakilishi wa UPDP amesema tayari kuna mwafaka wa kitaifa uliofikiwa kupitia kikosi kazi kilichoondoa dukuduku za kisiasa, ikiwamo wagombea kupita bila kupingwa.
Profesa Mkumbo wa CCM, akijibu hoja hiyo, amesema kususiwa kwa uchaguzi na chama kimoja, hakuwezi kuzuia mchakato wa kidemokrasia nchini.

Wakati huo huo, Ameir wa Demokrasia Makini Zanzibar, amesema nchi ina demokrasia ipo na anayesema haipo, anapaswa kuchunguzwa kwa makini.
“Serikali imeimarisha mazingira ya kisiasa, vyama vimepatiwa magari ya kampeni na vyombo vya habari vya umma vinatoa fursa sawa kwa wanasiasa wote,” amesema Ameir.
Hata hivyo, mdahalo huo umehitimishwa kwa wito kwa wananchi kusoma na kuchambua ilani za vyama kabla ya kufanya uamuzi wa kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo.