Arusha. Wanafunzi kutoka Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) kupitia kikundi chao cha Skyverse Solution, wameibuka washindi wa mashindano ya ujasiriamali na ubunifu ya Afrinnovate Youth Challenge baada ya kubuni mashine ya kubangua karanga.
Ubunifu huo umetajwa kuwa mkombozi kwa wakulima wadogo wa karanga, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia nguvu na muda mwingi kubangua zao hilo kwa mikono.
Mashindano hayo yamefanyika leo Jumapili, Septemba 28, 2025, katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), yakihusisha vikundi 10 kutoka vyuo vikuu mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar.
Mashine hiyo, iliyobuniwa ndani ya mwezi mmoja, imeelezwa kuwa suluhisho la moja kwa moja kwa changamoto za muda na nguvu zinazowakabili wakulima wadogo.
Akizungumza kwa niaba ya mwenzake, Schola Jonathan, mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Masuala ya Jinsia na Maendeleo ya Jamii, amesema wazo la kutengeneza mashine hiyo lilitokana na changamoto walizoziona miongoni mwa wakulima vijijini.
“Mashine hii inalenga kuongeza tija na kurahisisha kazi ya wakulima wadogo. Tayari tumewafikia wakulima zaidi ya 50 katika Wilaya ya Kondoa, Dodoma,” amesema Jonathan.
Ameongeza kuwa teknolojia na ubunifu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kujituma na kutumia mbinu bunifu kujiajiri badala ya kutegemea ajira.
“Vijana, tusisubiri kuajiriwa, lazima tuanze sasa kutumia teknolojia kutengeneza ajira zetu. Tuliona wakulima wadogo wakitumia muda mrefu kubangua karanga, ndiyo maana tulibuni mashine hii, na hadi sasa tumewafikia wakulima zaidi ya 50,” amesisitiza.
Kwa ushindi huo, kikundi hicho kimejipatia zawadi ya Dola 3,000 za Marekani (Sh 7.95 milioni) na kimepata nafasi ya kuwa mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya ubunifu na ujasiriamali ya vyuo vikuu barani Afrika, yatakayofanyika Desemba mwaka huu.
Mkurugenzi wa E3Empower Africa, Ji-Young Rhee, ambao wanatekeleza mradi wa Social Equity Program (SEP), amesema mashindano hayo yanakusudia kuwawezesha vijana kuibua suluhisho la changamoto za kijamii kupitia miradi bunifu yenye mchango wa kiuchumi na kijamii.
Katika mashindano hayo, washindi wa pili wamebuni mfumo unaotumia Akili Unde kuchunguza shinikizo la damu na ugonjwa wa kisukari, na washindi hao wamezawadiwa Dola 2,000 za Marekani (Sh 5.3 milioni). Washindi wa tatu walipata zawadi ya Dola 1,000 (Sh2.6 milioni) kwa bunifu yao.
Rhee amefafanua kuwa mchakato wa mashindano ulianza Aprili 2025 na kushirikisha vikundi 70 kutoka vyuo vikuu nchini, na baada ya mchujo, vikundi 10 vilifika fainali na kushindanishwa ili kumpata mshindi wa kuiwakilisha Tanzania katika ngazi ya Afrika.
Amesema pia kuwa vikundi vilivyofika hatua ya fainali vimepatiwa mafunzo ya uongozi, ubunifu na ujasiriamali kwa lengo la kuboresha miradi yao na kuhakikisha inaleta manufaa kwa jamii.