Moshi. Wakati saratani ya tezi dume ikitajwa kushika kasi katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, tafiti zinaonesha kuwa kati ya wanaume 470 waliopimwa mwaka 2023, 170 walikutwa na saratani hiyo bila wao kujua.
Hayo yameelezwa leo Septemba 28, 2025, na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa Yasiyoambukiza (KCRI) cha Hospitali ya KCMC, Profesa Blandina Mmbaga, wakati wa mkutano na waganga wa tiba asilia uliofanyika kata ya Kahe, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Aidha, Profesa Mmbaga amesema hali hiyo inaonesha umuhimu wa upimaji wa mapema, hasa kwa wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea, ili kubaini saratani hiyo kabla haijafikia hatua ya juu.
“Katika mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara tulipima zaidi ya watu 6,000, na katika hao tulipata wale waliokuwa na viashiria walikuwa zaidi ya 700. Hata hivyo, wale waliokuja katika vipimo vya mwisho vya kuchukuliwa kinyama na kupima, tulipata watu 470, na kati yao 170 walikuwa na saratani ya tezi dume bila wao kujua,” amesema Profesa Mmbaga.
Profesa Mmbaga ameongeza kuwa ni vema jamii ikawa na tabia ya kupima afya mara kwa mara, hata kama hakuna dalili za ugonjwa, ili mtu anapogundulika kuwa na tatizo achukue tahadhari na kupata matibabu mapema.
“Unapogundua ugonjwa wa aina yoyote mapema, inasaidia kuchukua tahadhari na kupata matibabu kwa wakati unaostahili,” amesema Profesa Mmbaga.
Profesa Mmbaga ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na Hospitali ya KCMC kwa kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa huduma ya tiba kwa wagonjwa wa saratani.
“Tunashukuru Mungu, Serikali yetu imetuona, na kwa kutuona imetusaidia kujenga jengo la mionzi hospitalini KCMC. Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuiwezesha KCMC kuwa na jengo hili la mionzi,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, Profesa Mmbaga amesema bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kuhusu saratani ya matiti, jambo ambalo wataendelea kushirikiana na waganga wa tiba asili ili kuwabaini wagonjwa.
“Bado uelewa wa saratani ya matiti ni mdogo, hasa kuhusu dalili na tiba. Hivyo, tukaona ni muhimu kutoa elimu na kuwafundisha waganga wa jadi jinsi ya kukagua titi lenye uvimbe na dalili za saratani pindi wananchi wanapokuwa wanatafuta huduma kwa waganga,” amesema.
Amesema: “Kwa kushirikiana na waganga wa jadi, miezi mitatu ya kwanza tulipata wagonjwa 20 ambao wamefanyiwa rufaa, na mpaka leo wagonjwa zaidi ya 65 wameletwa kwetu na hawa waganga wa jadi. Kuna baadhi walikuta wana saratani, wengine uvimbe wa kawaida, na wote wameweza kupata matibabu.”
Kwa upande wake, mtafiti kutoka KCRI, Dk Eliza Msoka, amesema uelewa wa saratani ya matiti bado ni mdogo, hivyo jamii inatakiwa kujifunza zaidi kuhusiana na dalili za ugonjwa huo.
“Tunasema saratani haina sababu ya moja kwa moja, isipokuwa kama mtu amezaliwa na kinasaba. Hata hivyo, matumizi ya tumbaku, unywaji wa pombe au sigara ni baadhi ya mambo yanayomsogeza mtu katika hatari ya kupata saratani,” amesema Dk Msoka.
Visababishi vingine vya saratani, amesema, tafiti mbalimbali zinaonesha uhusiano kati ya kuchelewa kupata mtoto wa kwanza na ongezeko la uwezekano wa kupata saratani ya matiti.
Amesisitiza umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi na uchunguzi wa mara kwa mara kwa wanawake wote, hususan wale walio kwenye kundi hilo la hatari.
“Pale ambapo mama anapopata mtoto wake wa kwanza akiwa na umri zaidi ya miaka 30, mama huyu anajisogeza zaidi karibu na hatari ya kupata saratani ya matiti,” amesema Dk Msoka.