Moshi. Watu watatu wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa baada ya gari aina ya Noah walilokuwa wakisafiria kutokea harusini mkoani Tanga, kugongana uso kwa uso na lori lenye tela.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema imetokea leo Jumapili Septemba 28, 2025 katika eneo la Njiapanda, wilayani hapa.
Mnzava amewataja waliofariki dunia kuwa ni Samwel Nyerembe (44) mkazi wa Bonite ambaye alikuwa dereva wa Noah, Rebeka Tarimo (29) mkazi wa Soweto na Farida Mazimu (40) mkazi wa Bonite.
Majeruhi ni Asia Lyimo (36) mkazi wa Bonite, Zainab Lyimo(38), Mariam Lyimo (39), Salome Oisso (36), Narahat Emmanuel mtoto wa miezi saba na Maira Lyimo mtoto, wote walikuwa kwenye Noah.
“Leo saa 10 alfajiri eneo la Njiapanda karibu na mnadani, tumepata ajali ya barabarani iliyohusisha magari mawili, Noah na gari kubwa aina ya lori,” amesema Mnzava.
Amefafanua kuwa Noah hiyo ilikuwa ikitokea Korogwe mkoani Tanga, huku lori likiwa linatokea Arusha kuelekea Tanga.
Majeruhi hao kwa mujibu wa Mnzava, wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC, huku miili ya marehemu ikihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti hospitalini hapo.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya amebainisha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, uliosababisha dereva wa Noah kushindwa kulimudu gari lake na hivyo kwenda kugongana na lori.
“Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi unaonesha chanzo cha ajali ni mwendo kasi uliosababisha dereva wa Noah kushindwa kumudu gari lake na kugongana na lori lililokuwa likitokea Arusha kuelekea Tanga,” amesema.
Mnzava amewataka madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuendesha kwa tahadhari kubwa ili kuepusha majanga yanayoweza kuepukika.
“Tunaendelea kuwasihi watumiaji wote wa barabara wakiwamo madereva kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani na kuendesha kwa tahadhari kwani uzembe mdogo unaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwamo vifo, majeruhi na uharibifu wa mali,” ameongeza.
Ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwaombea majeruhi wapate nafuu haraka.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kindi, Juma Mwisi amesema waliopata ajali walikuwa wakitoka kwenye sherehe ya harusi huko Tanga wakirejea Moshi.
“Ajali hii imesababisha vifo vya watu watatu na wengine kujeruhiwa. Walikuwa wakitokea kwenye harusi Tanga,” amesema Mwisi.