Wavuvi Igombe wapewa elimu ya mpigakura

Mwanza. Wavuvi wa mwalo wa Igombe, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, wamepewa elimu ya mpigakura na kuhamasishwa kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, 2025 ili kuchagua viongozi wanaowataka.

Elimu hiyo imetolewa leo Jumapili, Septemba 28, 2025, katika mwalo huo unaokadiriwa kuwa na wavuvi zaidi ya 5,000.

Mvuvi wa mazao ya samaki, Peter Bukanu, amesema elimu aliyoipata imemfahamisha kuwa vituo vya kupigia kura vitakuwa wazi kuanzia asubuhi hadi saa 10:00 jioni.

“Elimu niliyopewa imenieleza kuwa Oktoba 29 vituo vitakuwa wazi. Hata kama nimeenda ziwani na kurudi saa 11 jioni, bado nitapata nafasi ya kupiga kura, kisha nirejee nyumbani kusubiri matokeo,” amesema.

Amesema upigaji kura ni haki ya msingi na kura yake moja inaweza kuamua ushindi wa diwani au Rais anayemhitaji.

Ameongeza kuwa anatamani viongozi watakaochaguliwa waboreshe miundombinu, hususan barabara kutoka Igombe hadi uwanja wa ndege, iwekewe lami ili kuwe na usafiri wa uhakika wa daladala.

Mvuvi mwingine, Atanas Kamenye, amesema awali alijiandikisha kupiga kura mkoani Arusha, lakini kupitia elimu hiyo amegundua anaweza kuomba kupiga kura ya Rais katika kituo kingine.

“Nimejaza fomu ya maombi ya kupiga kura ya Rais hapa Igombe. Sisi wavuvi mara nyingi tunakosa fursa kama hizi kwa sababu vitu vingi hatuvielewi, lakini nashukuru kwa elimu hii imetufungua macho,” amesema.

Mchuuzi wa dagaa, Modesta Kidugu, amesema Oktoba 29 wanawake, wanaume na vijana wote wajitokeze kupiga kura ili kumchagua kiongozi bora atakayewafaa.

“Elimu ya mpigakura ni muhimu kwa sababu watu wanapofahamu utaratibu, hawawezi kukosa kushiriki,” amesema.

Ofisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Shilinde Malyagili, amesema elimu hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa kutoa hamasa kwa wananchi katika kata 19 za manispaa hiyo.

“Tunafahamu mwaka huu wa uchaguzi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imefanya maboresho mbalimbali katika sheria. Mojawapo ni kwamba mpigakura anaweza kuomba kupiga kura ya Rais katika kituo tofauti na alichojiandikisha.

“Septemba 15, 2025, tume ilitoa tangazo la kuruhusu wananchi waliopo maeneo tofauti kutuma maombi ya kupiga kura ya Rais. Zoezi hili lilianza Septemba 19 na litamalizika Oktoba 2, 2025,” amesema.

Amesema wananchi wanaweza kuwasilisha maombi hayo kupitia mtandao au kwa kujaza fomu, na tayari zaidi ya watu 20 kutoka Igombe wamejaza fomu hizo.

“Baada ya kujaza fomu, msimamizi wa uchaguzi huziingiza kwenye mfumo na mpiga kura hupokea ujumbe mfupi wa simu kuthibitisha. Baadaye tume ikishakubali, mpigakura atapata taarifa rasmi na siku ya uchaguzi ataweza kupiga kura katika kituo alichoomba,” amesema.

Malyagili amewataka wananchi kujitokeza pia kwenye mikutano ya kampeni ili wasikilize sera na kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi wanaoendana na matarajio yao.