Askofu Rugambwa azikwa Bukoba, huu hapa wasifu wake

Mwanza. Mwili wa Askofu Novatus Rugambwa umezikwa leo, Septemba 29, 2025, katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma, Bukoba mkoani Kagera.

Hayati Rugambwa amezikwa jirani na Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, Kardinali wa kwanza barani Afrika na aliyemrithisha jina lake pamoja na marehemu Askofu Nestor Timanywa, aliyemlea na kumpa daraja la upadri.

Misa Takatifu ya mazishi iliyohudhuriwa na maaskofu mbalimbali, viongozi wa dini na viongozi wa Serikali, imeongozwa na Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora.


Akizungumza wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya kumuombea na kumuaga askofu huyo aliyekuwa Balozi wa Papa, Kardinali Protase amesema kifo chake kimewasikitisha wengi, hasa baada ya afya yake kudhoofika kutokana na shambulio la kiharusi.

“Kwa sababu ya upendo wake mkubwa na usiobagua aliouonesha wakati akiwa hai, tumuone kama mtu aliyepita mautini na kuingia uzimani kwa mema mengi aliyoyafanya. Hakuwa mtu wa chuki wala mtu wa kifo, bali mtu wa furaha, matumaini na maisha kwa wengi aliokutana nao,” amesema.

Amesema alama nyingi zimeachwa na hivyo ni wajibu wa waumini kuendelea kumkumbuka na kumuombea ili Mwenyezi Mungu ampokee katika ufalme wake wa mbinguni.

Aidha, ameeleza kuwa mchango wake haukuishia Bukoba pekee, bali ulienea katika majimbo na jamii mbalimbali nchini Tanzania.

“Kitu kimoja nataka niseme, ni upendo wake. Mchango mkubwa aliutoa kuhakikisha Kanisa Kuu la Mama Bikira Maria Mwenye Huruma linaonekana zuri kama lilivyo leo.


“Nafurahi kuona tunamzika pale alipowatamani waliomtangulia, akiwemo Kardinali Laurean Rugambwa na Askofu Nestor Timanywa, aliyemlea na kumpa daraja la upadri,” amesema.

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa na Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Jovitus Mwijage, wamemshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya askofu huyo wakielezea yalijaa matendo ya upendo hasa kwa watoto maskini.

“Maisha yake yamekuwa shule ya imani, matumaini, upendo, uvumilivu, ujasiri, ukarimu na uaminifu kwa mafundisho ya kanisa. Amefanya mengi kimyakimya kwa kanisa, Tanzania na ulimwengu mzima,” amesema Askofu Mwijage.

Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Padri Prudence Mujwahuzi amesema alizaliwa Oktoba 8, 1957, kijiji cha Misengi, Parokia ya Maruku, Wilaya ya Bukoba.

Alibatizwa Novemba 1957, akapata komunio ya kwanza Novemba 22, 1964 na Kipaimara Julai 22, 1965.

Elimu ya msingi aliipata katika Shule ya Nyakatare (1963–1967) na Seminari Ndogo ya Mtakatifu Don Bosco Rutabo (1968–1971).

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Kardinali Protase Rugambwa akiongoza ibada ya misa ya mazishi ya Askofu Mkuu, Novatus Rugambwa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma, Bukoba mkoani Kagera leo Septemba 29, 2025.



Kati ya mwaka 1972 hadi 1975, alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne Seminari ya Rubya, kisha kidato cha tano na sita Seminari ya Mtakatifu Karoli Boromeo, Itaga, Jimbo Kuu Katoliki Tabora.

“Mwaka 1977 hadi 1978 alihudumu katika Jeshi la Kujenga Taifa, Bulombola Kigoma, kabla ya kujiunga na Seminari Kuu ya Mtakatifu Antoni, Ntungamo (1978–1980). Baadaye alisomea thiolojia Roma katika Chuo cha Kipapa Urbaniana.

Amesema mwaka 1984 hadi 1985 alifanya mwaka wa kichungaji katika Seminari ya Mtakatifu Maria Rubya na Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Ishamba.

Alipata daraja la Ushemasi Januari 6, 1986 na daraja la Upadri Julai 6, 1986 kwa mikono ya marehemu Askofu Nestor Timanywa.

Kwa mujibu wa Padri Mujwahuzi, Askofu Rugambwa alianza kuugua Oktoba 29, 2023, baada ya kupata kiharusi kikali akiwa kwenye utume wake wa kidiplomasia.

Alilazwa katika hospitali mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Wellington, Hospitali ya Kenepool na baadaye Hospitali ya Gemelli jijini Roma, Italia.


Amesema kutokana na hali yake kutokuwa nzuri kiafya, Julai 27, 2024 aliwasilisha barua ya kujiuzulu kutoka nafasi yake ya Balozi wa Kitume katika nchi alizokuwa akihudumia, hatua iliyokubaliwa rasmi na Vatican.

Amesema alifariki dunia jioni ya Septemba 16, 2025, akiwa na umri wa miaka 67, baada ya kulitumikia Kanisa kwa miaka 39 kama padri na miaka 15 kama askofu.

“Anakumbukwa kwa kuwa mtu wa imani na mwenye moyo wa sala. Alikuwa na bidii yake ya kichungaji akiwa ni mtu mtulivu bali mwingi wa nguvu katika kutetea mafundisho ya kweli ya kanisa… amekuwa mwenye upendo mkubwa kwa wale aliyekutana nao kila mara akiwa ni mwenye nia njema ya kuleta maendeleo.

 “Yeye ni mfano mzuri wa unyenyekevu unaoakisiwa katika mtazamo wake juu ya watu aliokabidhiwa. Alikuwa mtu mwenye ujuzi wa hali ya juu na alijaaliwa vipaji na vipawa vingi ambavyo hakuvificha. Kanisa Katoliki nchini Tanzania linajivunia zawadi ya mchungaji mwema aliyekuwa tayari hata kuhatarisha nafsi yake ili kustawisha injili katika mioyo ya watu,” amesema Padri Mujwahuzi.

Baada ya upadrisho, alihudumu mwaka mmoja Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Rushamba, kisha akajiunga na Chuo cha Kipapa cha Diplomasia (Pontifical Ecclesiastical Academy) mwaka 1987. Januari mosi, 1991 aliingia rasmi katika utume wa kidiplomasia wa Vatican.

Februari 20, 2010, Papa Benedict XVI alimteua kuwa Askofu Mkuu wa Tagaria na Balozi wa Kitume, akapewa daraja la uaskofu na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu Mkuu wa Vatican.

Balozi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Angelo Accattino amesema Askofu Rugambwa alitekeleza majukumu yake kwa uaminifu katika nchi mbalimbali. Akiwa Naibu wa Ubalozi wa Kitume, alitumwa katika nchi za Panama, Jamhuri ya Congo, Pakistan na Indonesia.


Baadaye alirudishwa Roma ambako alitekeleza majukumu ya Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Kichungaji kwa Wahamiaji na Wasafiri.

Mwaka 2010, Papa Benedict XVI alimteua kuwa Askofu Mkuu na Balozi wa Kitume, akapangiwa kuongoza uwakilishi wa Vatican katika nchi za Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sao Tome na Principe.

Askofu Accattino amesema alihudumu pia New Zealand pamoja na visiwa kadhaa vya Bahari ya Pasifiki ikiwemo Fiji, Samoa, Tonga, Kiribati, Vanuatu na Nauru, huku nchi ya Togo na Benini akihudumu kama Balozi wa Kitume.

“Katika kila utume wake, alijulikana kwa uaminifu na bidii kubwa ya kichungaji kama mwakilishi wa Baba Mtakatifu,” amesema Askofu Accattino.