Clara Luvanga anaitaka rekodi Saudia

BAADA ya kuingia kwenye kikosi bora cha wiki mara mbili kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Saudi Arabia, mshambuliaji wa Kitanzania, Clara Luvanga anayekipiga Al Nassr amesema huo ni mwanzo tu kwake.

Msimu mpya wa Ligi ya Wanawake Saudia umeanza na hadi sasa zimechezwa mechi tatu na nyota huyo ameingia kwenye kikosi bora cha wiki mara mbili.

Kwenye mechi alizocheza Al Nassr, mshambuliaji huyo wa timu ya taifa, Twiga Stars, alifunga mabao matano na kutoa asisti mbili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Clara alisema anatamani kuwa na muendelezo wa kufunga na kuisaidia timu hiyo na yeye binafsi kunyakua tuzo ya mfungaji bora.

“Najisikia furaha na nafikiri huo ni mwendelezo wa kile nilichokifanya misimu miwili iliyopita, natamani kiatu cha ufungaji bora msimu huu, na kila nachokifanya ni kwa ajili ya timu na malengo yangu binafsi,” alisema Clara.

Huu unakuwa msimu wa tatu kwa Luvanga kuitumikia Al Nassr tangu aliposajiliwa mwaka 2023 akitokea Dux Logrono ya Hispania, alikocheza kwa miezi mitatu tu na kupata shavu hilo.

Msimu wa kwanza alifunga mabao 11 na kutoa asisti saba na kusaidia kutetea ubingwa wa ligi hiyo na msimu uliopita aliweka kambani mabao 21 na asisti saba.