Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi miradi mikubwa ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya vipaumbele vya serikali atakayoongoza endapo atachaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Jumapili, Septemba 28, 2025, kwenye viwanja vya Polisi, Chalinze mkoani Pwani, Dkt. Samia alisema serikali yake itashirikiana na sekta binafsi kujenga barabara ya Kibaha–Chalinze–Morogoro, akibainisha kuwa ni barabara ya kimkakati wa uchumi na usafirishaji wa bidhaa.
“Hii ni barabara yenye tija kubwa kiuchumi, hivyo tutashirikiana na sekta binafsi ili wao watoe fedha sisi tufanye mambo mengine ya kipaumbele,” alisema Dkt. Samia.
Katika sekta ya afya, aliwaahidi wakazi wa Chalinze kuendeleza maboresho katika Hospitali ya Wilaya ya Chalinze, ikiwemo kuipandisha hadhi na kuhakikisha inatoa huduma zote muhimu. Aliwapongeza wananchi kwa kufanikisha kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Aidha, aliahidi kujenga shule mpya za msingi katika maeneo ya Chaua, Kibindu, Zigua na Changalikwa, sambamba na kuendeleza mpango wa elimu bila ada. Ameongeza kuwa serikali yake itatekeleza mpango wa bima ya afya kwa wote, ambapo majaribio yataanza ndani ya siku 100 za kwanza za serikali yake iwapo atachaguliwa.
Vilevile, Dkt. Samia aliahidi kufufua na kutekeleza mradi mkubwa wa Bandari ya Bagamoyo, akisema itajengwa katika eneo la Mbegani na utakuwa na gati za kisasa zenye uwezo wa kupokea meli kubwa zaidi ya zile zinazoingia Bandari ya Dar es Salaam.
“Tunakwenda kuijenga Bandari ya Bagamoyo katika eneo la Mbegani. Bandari hii itakuwa na gati za kisasa na ndefu ambazo zitakuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa zaidi ya Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Dkt. Samia.
Alisisitiza kuwa bandari hiyo itakuwa kitovu cha biashara ya kimataifa, na hivyo kuchochea uchumi wa taifa na kuongeza ajira kwa Watanzania.