::::::::
Tume ya Ushindani (FCC) ya Tanzania Bara na Tume ya Ushindani wa Haki Zanzibar (ZFCC) zimetia saini mkataba wa makubaliano wenye lengo la kuhakikisha kuwepo kwa mazingira ya ushindani wa haki katika masoko na kulinda maslahi ya walaji ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makubaliano hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano wa kisheria, kitaalamu na kiutendaji kati ya taasisi hizo mbili katika kudhibiti vitendo vya ushindani usio wa haki pamoja na ukiukwaji wa haki za walaji, kwa mujibu wa sheria za pande zote mbili za Muungano.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdalah, alisema hatua hiyo ni ya kihistoria na ya kimkakati kwa maendeleo ya mfumo wa soko huria na ulinzi wa watumiaji wa bidhaa na huduma.
“Makubaliano haya yanaweka msingi thabiti wa utekelezaji wa shughuli za pamoja kati ya taasisi hizi mbili. FCC na ZFCC zinapaswa kuteua watu au timu maalum kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano haya,” alisema Dkt. Hashil.
Aliongeza kuwa ndani ya kipindi kisichozidi miezi mitatu, au hata chini ya mwezi mmoja, nyaraka muhimu kama ramani ya utekelezaji (roadmap) na mpango kazi zinapaswa ziwe tayari na zianze kutumika mara moja.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, alisema kuwa mkataba huo unaashiria mshikamano wa kitasisi kati ya pande hizo mbili na unaonyesha dhamira ya pamoja katika kulinda masoko na haki za walaji nchini.
“Ushirikiano huu ni hatua ya kimkakati inayolenga kuongeza nguvu ya pamoja katika kukabiliana na changamoto kama ushindani usio wa haki na ukiukwaji wa haki za walaji,” alisema Bi. Ngasongwa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa ZFCC, Bi. Aliyah Juma, alisisitiza kuwa tume hiyo iko tayari kushirikiana kikamilifu na FCC kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa manufaa ya walaji na wadau wa soko kwa ujumla.
Makubaliano hayo yanakuja wakati serikali inaendelea kuimarisha taasisi zake katika kuhakikisha kuwa masoko nchini yanaendeshwa kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia ushindani unaowawezesha walaji kupata bidhaa na huduma bora kwa bei stahiki.
PICHA ZOTE NA JAMES SAVATORY