ALIYEKUWA mshambuliaji wa Simba na Yanga, Mkongomani Jean Baleke, anakaribia kujiunga na kikosi cha Al-Khums ya Libya, baada ya nyota huyo kudaiwa amekubaliana masilahi binafsi na timu hiyo ambayo imeonyesha nia ya kumhitaji.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Libya, zinaeleza Baleke aliyeachana na Yanga baada ya mabosi wa timu hiyo kutoridhishwa na kiwango chake, kwa sasa anakaribia kujiunga na Al-Khums baada ya dili la kujiunga na Rayon Sports kutoka Rwanda kukwama.
Nyota huyo hadi anaondoka Yanga aliifungia bao moja la Ligi Kuu, alilolifunga dakika ya 24, wakati timu hiyo iliposhinda 1-0 dhidi ya Coastal Union, Oktoba 26, 2024 pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Baleke alitua nchini kwa mara ya kwanza, Januari 15, 2023 na kujiunga na kikosi cha Simba akitokea Nejmeh SC ya Lebanon aliyokuwa anaichezea kwa mkopo akitokea TP Mazembe ya kwao DR Congo na kuonyesha kiwango bora kwa muda mfupi aliocheza.
Kwa msimu wa 2022-2023, Baleke aliifungia Simba mabao manane ya Ligi Kuu Bara katika kipindi cha miezi sita aliochezea kikosi hicho, huku idadi hiyo ya mabao ikiwa ni sambamba na aliyofunga pia nyota huyo kwa msimu uliofuata wa 2023-2024.
Awali nyota huyo alifanya mazungumzo na Mtibwa Sugar iliyoonyesha nia ya kumhitaji kwa ajili ya msimu huu wa 2025-2026, ingawa suala la masilahi binafsi baina ya pande hizo mbili yalishindwa kufikia mwafaka na dili hilo kushindwa kukamilika.