Kesi ya kikatiba kupinga ulimaji, matumizi ya tumbaku Tanzania yatupwa

Dodoma. Mahakama Kuu imeitupa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Watanzania wanne wakiibana Serikali isitishe kilimo na matumizi ya tumbaku, ikiwamo uvutaji wa sigara, kutokana na dosari za kisheria zilizobainika wakati wa kulipia nyaraka.

Uamuzi wa kulitupa shauri hilo umetolewa Septemba 25, 2025, na nakala ya hukumu kupatikana leo Septemba 29. Katika kuhakikisha afya ya Watanzania haihatarishwi na bidhaa za tumbaku na kilimo chake, walifungua kesi ya kikatiba dhidi ya Waziri wa Afya, Waziri wa Kilimo, Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Waliomba Mahakama itoe amri mbalimbali dhidi ya wadaiwa hao kwa kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na vyombo vingine vya kimataifa vinavyohusiana na tumbaku, ambapo Tanzania ni mwanachama.

Kupitia shauri hilo, walilalamika kwamba wadaiwa wana jukumu takatifu la kuhakikisha mazingira safi na yenye afya, kwamba kilimo na uzalishaji wa tumbaku sio endelevu, kinaharibu mazingira, kunadhuru afya na kuzidisha umaskini.

Mbali na hilo, walidai pia kuwa kilimo cha tumbaku ni mzigo wa uchumi, na Serikali imeshindwa kuwalinda wafanyakazi na wasiofanyakazi katika kilimo hicho, pamoja na kushindwa kuwalinda wasiovuta sigara na umma wa Watanzania kwa ujumla.

Pia waliwalalamikia wadaiwa kwa kushindwa kusimamia hatua za usimamizi na kushindwa kutunga sheria kali za tumbaku, ikiwemo kutekeleza kanuni za World Health Organization Framework Convention on Tobacco Control (WHO FCTC).

Walitaka Mahakama iilazimishe Serikali kusitisha kilimo cha tumbaku ndani ya miaka mitatu, kuanzisha njia mbadala za kiuchumi kwa ajili ya kuendeleza maisha, na kuheshimu mkataba wa WHO FCTC.

Waliomba pia kutotoza adhabu na kodi kubwa, kuondoa ruzuku kwa kilimo cha tumbaku, na kutoa mrejesho wa utekelezaji wa amri hizo ndani ya mwaka mmoja.

Majaji walivyoibua dosari

Dosari hizo ziliibuliwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma—Abdi Kagomba, Suleiman Hassan na Dk Angelo Rumisha – siku chache kabla ya hukumu kutolewa, na walilazimika kuiita upande wa wadai.

Awali, hukumu ilikuwa imepangwa kutolewa Septemba 15, 2025, lakini majaji walibaini dosari katika mchakato wa kuandika hukumu.

Katika uamuzi wao wa kulitupa shauri hilo, majaji hao walisema Julai 22, 2025, walizielekeza pande mbili katika shauri hilo, kuwasilisha mawasilisho ya mwisho huku wakitakiwa kuwasilisha wasilisho kuu Julai 29, 2025.

Wakiamini kuwa pande zote zilitii amri hiyo, Mahakama ilipanga tarehe ya hukumu kuwa Septemba 5, 2025 lakini wakati wakiandaa hukumu, hawakuona wasilisho kuu la wadai kama Mahakama ilivyoagiza Julai 22, 2025.

Hivyo, wakiziita pande mbili zifike mbele yao Septemba 12, 2025, ili kufanya mawasilisho ya kama waleta madai walikuwa wamewasilisha wasilisho kuu (chief submission) kama Mahakama ilivyoagiza, na watoe uthibitisho huo.

Siku hiyo wadai waliwakilishwa na mawakili Dk Rugemeliza Nshala, Ibrahim Mcharo na Hamis Mayombo huku wadaiwa wakiwakilishwa wakili mwandamizi wa Serikali Narindwa Sekimanga akisaidiwa na Victoria Lugendo na Mariam Selemi.

Dk Nshala alieleza wakati wanawasilisha wasilisho kuu kupitia mfumo wa mahakama (e-case filing), walishindwa kupata namba ya malipo kwa ajili ya kulipa ada ya mahakama na walisubiri kwa muda mrefu bila mafanikio.

Wakati wanaomba kibali cha kuwasilisha wasilisho la ziada (rejoinder), walijulishwa kuwa wasilisho kuu lilikuwa halionekani katika mfumo na hivyo wakili Mayombo akalazimika kuomba namba nyingine ya malipo.

Walipata namba mbili tofauti, ambazo walizilipa, na awali waliambiwa namba moja ni kwa ajili ya wasilisho kuu na nyingine ilikuwa ni kwa ajili ya wasilisho la ziada lakini baadaye waligundua zote zilikuwa ni kwa ajili ya rejoinder.

Dk Nshala aliendelea kueleza kuwa waliwasilisha suala hilo kwa maofisa wa mahakama, hivyo wadai wasiwajibike kuadhibiwa kwa makosa ambayo hawakuyafanya wao hivyo wakaomba Mahakama iokoe jahazi katika hilo.

Wakati usikilizwaji unaendelea kwa njia ya mtandao (virtually), Mahakama ilimtaka Dk Nshala kuonesha ‘screen’ kuthibitisha kama kweli wasilisho hilo kuu liliwasilishwa, ambapo alisema aliyefanya hilo alikuwa ni wakili Mayombo.

Wakili Mayombo aliposhirikisha screen yake ilionekana wazi kuwa wasilisho hilo lilisomeka ‘pending bill’ ikimaanisha lilikuwa bado halijapokelewa.

Kwa upande wake, wakili mwandamizi wa Serikali, Narindwa alijenga hoja kuwa kimsingi wadai hawakutekeleza amri ya mahakama ya kuwasilisha wasilisho kuu na kwamba kushindwa huko kulikuwa kubaya na hakuwezi kusamehewa.

Aliongeza kulingana na kanuni inayosimamia mfumo wa e-filing, upande unaokutana na changamoto unapaswa kuwasiliana na msajili ndani ya saa 15 ili kutatua changamoto, lakini wao wanadai karani aliwapa namba zingine za malipo.

Wakili huyo alisisitiza kanuni ziko wazi waombaji walipaswa kutafuta uingiliaji kati wa msajili jambo ambalo hawakufanya hivyo na kueleza kuwa kushindwa kutekeleza amri ya mahakama ni kuwa wameshindwa kusimamia kesi yao.

Alieleza kuwa jambo ambalo Mahakama inaweza kulifanya ni kulitupa shauri hilo na kwamba wadai wameshindwa kushawishi nia yao ya kuendesha shauri hilo na hawakutakiwa kusubiri hadi mahakama ndio iibue dosari ilizoziibua.

Majaji hao walisema kumbukumbu za mfumo wa e-filing uko wazi kuwa sio Dk Nshala wala wakili Mayombo aliyewasilisha wasilisho kuu kama ilivyoamriwa.

Badala yake, walisema mfumo unaonesha kuwa mtu aitwaye Janeth Kazimoto aliandaa wasilisho hilo na kuingiza kwenye mfumo kwa ajili ya msajili kuipitia.

Majaji walisema Agosti 1,2025, namba ya malipo 991401404364 ya Sh20,000 ilitengenezwa kwa ajili ya Kazimoto kufanya wasilisho hilo na namba hiyo iliendelea kuwa hai hadi Agosti 6, 2025 ilipoisha muda wake wa matumizi.

“Katika hatua hiyo, wasilisho hilo liliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Kazimoto. Kama ada hiyo ingelipwa, wasilisho hilo lingekuwa limeenda hatua inayofuata na lingeonekana katika kumbukumbu za mahakama na maji wangeliona,” walisema.

“Kama namba ya malipo imeisha muda wake wa matumizi, mdai anawajibuka kutengeneza nyingine mpya ili kukamilisha kuwasilisha wasilisho hilo, lakini hii hatua haikuchukuliwa na mdai,” walieleza majaji katika uamuzi wao.

“Hii inafuatia sasa kuwa ugumu ambao Dk Nshala anasema waliupitia hauthibitiki katika mfumo wa kesi. Namba ya malipo ilitolewa lakini ada haukulipwa na uwasilishaji wa nyaraka hiyo haukuvuka msitari wa mwisho,” walieleza.

Majaji hao walikuwa na maoni kuwa nyaraka haiwezi kuhesabika iliwasilishwa mahakamani kama nyaraka hiyo haiwezi kufikiwa na Jaji na upande wa pili wa kesi.

“Hatuna nia ya kurejesha gurudumu. Katika suala hili, kuna uamuzi mmoja uko wazi mbele yetu, kwa bahati mbaya ingawa inaweza kuwa, na uamuzi huo ni kuliondoa shauri hili na hapa tunatamka shauri hili limeondolewa,”walisema.

Majaji hao walisema kwa kuwa suala la dosari za kisheria katika shauri hilo ziliibuliwa na Mahakama yenyewe, kila upande utabeba gharama zake za kesi.