Kipa Dodoma Jiji aipigia hesabu Taifa Stars

KIPA wa Dodoma Jiji, Ally Salim amesema japo ni mapema kwa sasa kuanza kutamba, lakini nafasi anayopata ya kucheza katika timu hiyo, imempa matumaini makubwa ya kumrejesha tena kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.

Kipa huyo juzi alicheza mechi ya tatu ya Ligi Kuu akiwa na Dodoma na kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union kitu kilichompa faraja kwani tangu ajiunge akitokea Simba amekuwa akiaminika na makocha.

Salim alisema Taifa Stars ni ya kila mchezaji wa Kitanzania na anayekuwa katika kiwango kizuri ndiye anayepata nafasi ya kuitumikia, jambo linalomfanya ajitume na kuhakikisha kiwango chake kinakuwa juu.

“Mchezaji anayepafomu ndiye anakuwa na nafasi ya kulitumikia taifa lake, lakini jambo la msingi kwangu ni kuhakikisha najituma ili timu iweze kufikia malengo yake ndipo mengine mazuri yanaweza kuonekana,” alisema Salim na kuongeza;

“Natambua Ligi Kuu ya msimu huu siyo nyepesi, timu zimesajili vizuri, wachezaji wanapambana kuonyesha viwango vyao, hilo linaonyesha ubora wa kila mchezaji anayejituma.”

Salim alisema ushirikiano na wachezaji wenzake, anaamini unakwenda kuwa msimu wa mafanikio kwa upande wake na timu kwa jumla.

“Ushirikiano katika timu ndiyo chanzo cha mafanikio, kila mtu akipambana kwa nafasi yake ni rahisi kupata ushindi. Nikikaa na wachezaji wenzangu naona namna ambavyo kila mtu alivyo na hamu ya kufanya makubwa, hilo linanipa nguvu ya kuuona utakuwa msimu bora,” alisema kipa huyo.