TIMU ya Malindi kutoka Unguja, imefanikiwa kuvuna alama tatu kwa kuifunga Chipukizi bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Zanzibar iliyochezwa Septemba 27, 2025 kwenye Uwanja Gombani uliopo kisiwani Pemba.
Bao hilo lilifungwa na Tchakei Moucheri dakika 15 akimalizia pasi ya Ramadhan Mponda ambapo lilidumu hadi timu hizo zinakwenda mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa Chipukizi kupambana kusawazisha bao hilo, lakini ilishindwa kufanikisha hilo na kujikuta ikianza ligi kwa kichapo cha nyumbani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Msaidizi wa Malindi, Mohamed Salah ‘Richkard’ amesema mechi hiyo ilikuwa ngumu lakini wachezaji walijituma vya kutosha kuhakikisha wanapata ushindi.

MLAND 01
Richkard amesema mambo yote ambayo walikuwa wanayafanyia kazi uwanja wa mazoezi ndiyo yaliyorahisisha kuibuka na ushindi huo, hivyo hilo ni jambo la faraja upande wao.
Timu hizo huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Zanzibar iliyoanza Septemba 25, 2025.