Mwili wa Hayati Askofu Mkuu Novatus Rugambwa, aliyefariki hivi karibuni, uliwasili leo katika Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Huruma, Jimbo Katoliki Bukoba, na kupokelewa kwa heshima kubwa na waumini pamoja na viongozi wa Kanisa Katoliki.
Waumini kwa mamia walijitokeza kuupokea mwili huo, huku ibada maalum ya kumuombea ikiongozwa na viongozi wa Kanisa, ikihudhuriwa pia na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa madhehebu mbalimbali pamoja na wananchi.
Katika hotuba zao, viongozi wa dini walimsifu Hayati Askofu Mkuu Rugambwa kwa uongozi wake thabiti, hekima, na moyo wa utumishi uliogusa maisha ya wengi, si tu ndani ya Kanisa, bali pia katika jamii kwa ujumla.
Waumini waliendelea kumwombea marehemu apumzike katika amani ya Bwana, huku taratibu za mazishi zikitarajiwa kuendelea katika siku chache zijazo.