BAADA ya Denis Kitambi kutoonekana na kikosi cha Fountain Gate katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Septemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, taarifa zinabainisha amemalizana na uongozi wa klabu hiyo huku sababu ya kufanyika hayo ikiwekwa wazi.
Kitambi aliyeonekana kwa mara ya kwanza akikiongoza kikosi hicho Agosti 31, 2025 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Tabora United, huku akitambulishwa rasmi Septemba 20, 2025, amefanikiwa kuiongoza Fountain Gate katika michezo miwili ya Ligi Kuu Bara na kupoteza yote dhidi ya Mbeya City (1-0) na Simba (3-0).
Taarifa kutoka kwa mtu wa karibu na kocha huyo, zinabainisha kwamba, Kitambi amefikia makubaliana ya kuachana na Fountain Gate kutokana na sababu zake binafasi.
“Ameondoka kwa sababu ya kikosi kuwa na kiwango cha chini kutokana na mambo mengi ambayo yanaendelea ndani ya timu, jambo hilo hawezi kuliweka hilo hadharani.

“Ametaka kutafuta changamoto mpya, kwani ana malengo makubwa ya kuifundisha timu na kuifikisha mbali, ila ameona hawezi kutoboa ndani ya Fountain,” alisema mtu huyo.
Kiongozi mmoja wa Fountain Gate, ameiambia Mwanaspoti kuwa: “Taarifa zitatolewa katika mitandao ya kijamii, kuna mambo yanawekwa sawa kama viongozi.”
Fountain Gate haijaanza msimu vizuri kufuatia kukumbana na changamoto kwenye mfumo wa usajili ambapo ina wachezaji 14 pekee waliofanikiwa kusajiliwa kwa wakati ambao ndiyo waliohusika kwenye mechi tatu za ligi ilizocheza.
Hali hiyo inatajwa kuwa ndiyo miongoni mwa sababu za Kitambi kuishia njiani kwani licha ya timu kucheza vizuri, lakini inakumbana na changamoto hiyo inayoweza kudumu hadi Desemba 2025 kipindi cha usajili wa dirisha dogo.
Katika mchezo wa jana Septemba 28, 2025 ambao Fountain Gate ilipoteza ugenini kwa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, kikosi hicho kiliongozwa na kocha msaidizi, Mohamed Ismail ‘Laizer.

Kitambi kabla ya kutua Fountain Gate ikiwa ni siku chache baada ya klabu hiyo kuachana na Mnigeria, Ortega Deniran, amewahi kuzifundisha Ndanda, Simba, Namungo, Geita Gold, Azam FC na AFC Leopard ya Kenya.
Wakati hali ikiwa hivyo Fountain Gate, kule Coastal Union napo kuna taarifa zinabainisha klabu hiyo imefikia makubaliano ya kuachana na kocha wake mkuu, Ally Mohammed Ameir.
Ameir ameiongoza Coastal katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara msimu huu akishinda moja dhidi ya Tanzania Prisons (1-0), kisha kupoteza 2-1 mbele ya JKT Tanzania na kulala 2-0 kwa Dodoma Jiji.
Mara baada ya vipigo hivyo, zilienea tetesi kwamba mabosi wa klabu hiyo walikuwa mbioni kumpiga chini Ameir na mapema jana asubuhi chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Coastal kimelithibitishia Mwanaspoti kuwa ni kweli uongozi umekubaliana na kocha kusitisha mkataba.
“Tumemalizana na kocha, muda wowote kuanzia sasa taarifa itatoa taarifa kuhusiana na hilo, na tayari tumeshafanya mawasiliano na Muya (Mohamed) ndiye atakayekuwa kocha mkuu.
“Ni mazungumzo ya pande zote mbili yamefanyika na tumefikia makubaliano ya kusitisha mkataba, hivyo hakuna kitu kilichoharibika na uamuzi tuliouchukua ni kwa maslahi mapana ya klabu,” kilisema chanzo hicho.

Kuondoka kwa Ameir, Coastal Union inatajwa kumpa nafasi hiyo kocha wa zamani wa Fountain Gate, Mohamed Muya.
Mwanaspoti imefanya jitihada za kumtafuta kocha Muya, ili kupata ukweli wa taarifa hizo ambapo amesema: “Nafikiri uongozi ndio watu sahihi wa kutoa hizi taarifa, sipo katika nafasi nzuri ya kuzungumzia hilo, naomba uwapigie wao.”
Muya aliyewahi kuzifundisha Dodoma Jiji na Fountain Gate, anatua Coastal Union baada ya kumalizana na Geita Gold aliyoiongoza msimu uliopita kwenye Ligi ya Championship. Geita Gold kwa sasa inanolewa na Zuberi Katwila.
Hadi kufikia sasa ikiwa ni raundi ya tatu ya Ligi Kuu Bara 2025-2026, timu tatu zimeshabadilisha mabenchi yao ya ufundi kutokana na sababu mbalimbali.
Alianza Fadlu Davids kufikia makubaliano ya kuachana na Simba ambapo taarifa ilitolewa rasmi Septemba 22, 2025.
Fadlu hakufanikiwa kuiongoza Simba katika mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara, zaidi ya kusimamia Ngao ya Jamii timu hiyo ikipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga, kisha ushindi wa 1-0 mbele ya Gaborone United kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali.
Siku chache baada ya Fadlu kuondoka Simba, ndipo Kitambi na Ameir wamefuatia.