Sababu za Tanga Cement kuweka hisa zake sokoni

Dar es Salaam. Kampuni ya Tanga Cement yaweka sokoni hisa stahiki zenye thamani ya Sh204 bilioni ikilenga kusaidia kulipa madeni ya nje.

Pia pesa zitakazopatikana zinatarajia kukuza mtaji utakaosaidia kuongeza uzalishaji na usambazaji wa bidhaa ya saruji ndani na nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mauzo ya hisa hizo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amesema kiasi hicho cha thamani ya hisa stahiki ni kikubwa kuwahi kutokea katika historia ya masoko ya mitaji.

“Kwa mara ya mwisho mwaka 2015 hisa stahiki ziliuzwa na Benki ya CRDB zikiwa na thamani ya Sh150 bilioni,” amesema Mkama.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa saruji nchini na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.

Pia amesema itasaidia kuongeza mapato na fursa za uwekezaji kwa makampuni na hata wananchi wa kawaida.

Hivyo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa kampuni mbalimbali kutumia fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji kwa kuuza hisa kwa umma.

Mkurugenzi Mtendaji kampuni ya Tanga Cementm, Alfonso Velez (kulia) akimkabizi kitabu cha waraka wa matarajio ya kampuni hiyo, Nicodemus Mkama, katika uzinduzi wa mauzo ya hisa stahiki kwa wawekezaji katika kampuni ya saruji ya Tanga Cement leo Septemba 29, 2025 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Cement, Alfonso Velez amesema hisa hizo zitaanza kuuzwa rasmi kuanzia leo Septemba 29, 2025 hadi 24 Oktoba 2025 kwa Sh1600 kwa kila hisa.

Velez amesema bei hiyo ni ya punguzo kwa muda huo wa takribani mwezi mmoja.

“Baada ya muda huo kupita hisa hizo zitauzwa kwa gharama ya awali ya Sh2,590 kwa kila hisa, punguzo hilo limelenga kuwavuta wawekezaji wengi zaidi kuanzia taasisi hadi watu binafsi, jambo litakalosaidia kupanua ushiriki wa soko na kuimarisha imani katika masoko ya hisa nchini,” amesema.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo imelenga kuongeza ufanisi ili kuendana na kasi ya ukuaji wa soko la saruji ndani na nje ya nchi.

Naye Mkuu wa Idara ya Ushauri wa Fedha kutoka Kampuni ya iTrust Finance, Frank Bunuma amesema taratibu zote za kisheria zimezingatiwa katika uuzaji wa hisa hizo.

“Mchakato wa uuzaji wa hisa hizo umepata idhini ya mamlaka husika baada ya kukidhi matakwa ya kisheria,” amesema.