Samia aahidi makubwa Pangani, akimsifu Aweso

Tanga. Mgombea urais kupitia CCM Samia Suluhu Hassan amesema mgombea ubunge wa jimbo la Pangani Jumaa Aweso amefanya kazi kubwa iliyofanya upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85.

Amesema katika kipindi kijacho cha miaka mitano mpango wa Serikali ni kuhakikisha inamaliza changamoto ya maji kwenye maeneo yote yaliyosalia ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na salama.

Samia ameyasema hayo leo Septemba 29.2025 katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika wilaya ya Handeni mkoani Tanga ambao aliutumia kumnadi mgombea wa ubunge wa jimbo hilo ambaye ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

“Nilimpa kazi Aweso na nataka niwahakikishie kuwa kijana wenu hajazingua, ndiyo maana kwenye usambazaji wa maji tumefikia asilimia 85 kitaifa na miaka mitano ijayo tunakwenda kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama Tanzania nzima,”.


Mgombea huyo wa CCM amesema endapo atapata ridhaa ya miaka mitano mengine itaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji na kusogeza huduma hiyo muhimu kwa wananchi.

Kuhusu miundombinu amesema Serikali yake itaendeleza mpango wa kuufungua ukanda wa Pwani kiuchumi na kupunguza gharama za usafiri kwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya Bagamoyo -Pangani hadi Tanga.

Amesema ujenzi wa kipande cha kilomita 50 cha Pangani- Tanga kimefikia asilimia 75 wakati kipande cha Saadan – Makurunge chenye kilomita 95 ujenzi wake umefikia asilimia 50.

“Ahadi yetu ni kukamilisha barabara hii na si muda mrefu tutaanza kufaidi matunda yake,” amesema Samia.


Kwenye sekta ya uvuvi amesema mpango uliopo ni kuendelea kuwashika mkono wa wavuvi na kuongeza kipato chao kama ambavyo  tayari wilaya ya Pangani imeshaanza ujenzi wa soko la kimataifa la samaki litakalokuwa na vifaa vya kisasa vya kuhifadhia samaki na vile vya kukaushia dagaa.

Kwenye sekta ya mifugo amesema  mpango ulipo ni kuhakikisha wafugaji wanauza mifugo na mazao ya mifugo nje ya nchi hivyo Serikali  itaendeleza mpango wa ruzuku kwa chanjo, unaolenga kuku na mifugo mikubwa.

“Awali tulikuwa tunapata changamoto ya kupata masoko ya kimataifa kwa nyama na mifugo hai kwa sababu tulikosa vyeti vya kiafya vinavyokidhi viwango vya dunia. Safari hii tumeanzisha chanjo kwa ruzuku ili kuhakikisha mifugo yetu inakidhi viwango hivyo,” amesema.

Kufuatia hilo amewataka   wafugaji kuunga mkono mpango huo wa chanjo na kufuata taratibu zote ili waweze kunufaika na masoko mapya ya nje ya nchi kwa kile alichoeleza kufanikiwa kwa wavuvi ni kufanikiwa kwa Taifa:


Mgombea huyo alitumia  fursa hiyo kuwaomba wana Pangani kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, kwa ajili ya kuwapigia kura wagombea wa CCM.

“Ombi langu kwenu Oktoba 29 tutoke pamoja twende kwenye vituo vya kupiga kura, balozi usitoke peke yako toka na nyumba zako twende pamoja. Niwaombe vijana wote watoke kwenda kupiga kura,”

Akizungumza kwenye mkutano huo mgombea ubunge viti maalumu mkoani Tanga, Husna Shekiboko  amesema hatua ya kuweka vyuo vya ufundi kwenye wilaya zote za mkoa huo imesaidia vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.

“Muda si mrefu katika vituo vya mabasi kote nchini vijana kutoka Tanga wataanza kuadimika, maana ilikuwa wanaonekana wao ndiyo hawana shughuli za kufanya lakini sasa tuna vyuo wanapata ujuzi unaowawezesha kujiajiri.

“Mbali na hilo la vijana wetu, tumeweza kupata huduma zote za kijamii kuanzia maji, elimu, huduma za afya hadi mikopo kwa sababu hiyo wanawake wa Tanga tumeshafanya uamuzi itakapofika Oktoba kura zetu zote ni kwa Samia aendeleze aliyoyaanza,” amesema Husna.

Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo la Pangani Jumaa Aweso amesema Wilaya ya Pangani ilikuwa na changamoto kubwa ya uwekezaji kwenye elimu hivyo vijana wengi walikuwa hawasomi.

Amesema katika kipindi cha miaka 10 uwekezaji umefanyika kwa kujenga shule na kuhamasisha wazazi kusomesha watoto na mafanikio yameanza kuonekana.

“Ilikuwa ngumu kuona kijana wa Pangani anafanya kazi kwenye taasisi kubwa, ukweli ni kwamba elimu ilikuwa chini lakini sasa uwekezaji umefanyika kwenye sekta hii watoto wote wanasoma hata wale wanaotoka kwenye familia duni kabisa,” amesema

Mgombea ubunge huyo ameomba Serikali ifungue usafiri wa njia ya maji kwa kuweka boti ya haraka  ili kuwezesha shughuli za utalii katika wilaya hiyo iliyopakana na  maeneo mbalimbali yenye vivutio.

Akizungumza kwenye mkutano huo mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM, Nape Nnauye amesema vikao vya CCM vilivyopitisha jina la Samia kuwa mgombea urais havikukurupuka, sio bahati mbaya bali ilifanyika tathmini ya kina na kujiridhisha kuwa anatosha na mzalendo.

Amesema tathmini hiyo ilionesha Samia ni muumini thabiti wa utu wa mwanadamu na ndiyo sababu vikao vikaamua kumpendekeza awanie kwenye nafasi hiyo.

“Samia alipoingia madarakani alikuta miradi iliyokwishaanza, aliendeleza ipo aliyokamilisha na kuanzisha mingine ya ziada. Alikuta nchi inakusanya Sh18 trilioni ila kutokana na usimamizi wake zimefika Sh32 trilioni ambazo zimekuja kwenye miradi  ya maendeleo.

“Kwa haya na mengine mengi yaliyofanyika hatuna sababu ya kuwasikiliza wanaotushawishi Oktoba 29 tusiende kupiga kura, tusifanye kosa hilo niwaombe siku hiyo ikifika tuirudishe CCM katika ngazi zote,” amesema Nape.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro amesema chama hicho kimemteua Samia kikitambua kuwa ni mgombea ambaye amekamilika kwenye uongozi na ana rekodi ya utendaji na mafanikio. 

“Mgombea wetu anatosha kwenye kila idara, anakuja na utu, Oktoba 29 tutakwenda kupigia kura maendeleo na utu wa Mtanzania. Tuna kila sababu ya kumpa miaka mitano mingine ili aendeleze kazi nzuri aliyoianza,” amesema Dk Asha-Rose.