BAADA ya kufuzu raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa chini ya kaimu kocha mkuu, Hemed Suleiman ‘Morocco’ uongozi wa Simba umetuma maombi ya kumhitaji kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally ili kuongeza nguvu benchi la timu hiyo kama kocha msaidizi.
Simba iliyofikia makubaliano ya kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids na kumkaimisha Morocco bado ipo katika harakati za kutafuta kocha mkuu mpya.

Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti, klabu hiyo imefanya mazungumzo na kocha mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally ili kumuongeza katika benchi la ufundi kama kocha msaidizi, kusaidiana na Morocco pamoja na Seleman Matola.
“Simba tayari imempa ofa rasmi kocha huyo na mchakato unaendelea mambo yakienda kama walivyopanga, atajiunga na timu haraka na kukaa benchi katika mechi ya ligi dhidi ya Namungo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kuhusu suala la kocha mkuu pia ni suala la muda tu, tunaendelea kupambana kutafuta na kuna maombi mengi tumeyapokea kutoka kwa makocha wenye CV kubwa muda ukifika wanasimba watamfahamu kocha.”
Mtoa taarifa huyo amesema mchakato wa kumtafuta Ahmad ni baada ya makubaliano na kocha Morocco kukamilika na wanaamini mpango wao ukienda sawa kocha huyo atakuwa sehemu ya benchi lao msimu huu.

Simba hadi mechi ya jana iliyoambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Gaborone United na kutinga hatua inayofuata kwa faida ya ushindi wa bao 1-0 iliyopata ugenini na sasa inajipanga kukutana na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini ili kusaka nafasi ya kutinga makundi.
Msimu uliopita chini ya Fadlu, Simba ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa jumla ya mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco.