Na Pamela Mollel,Arusha
Taasisi ya Na Simama na Mama nchini Tanzania, yenye malengo ya kuinua wanawake katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, imepanga kushiriki kwenye maandamano ya amani kwa lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi kwa amani na mshikamano.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea siku ya uzinduzi wa taasisi hiyo kwa Kanda ya Kaskazini, Mwenyekiti wa Kanda, Monica Suleman, alisema maandamano hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mshikikano wa kijamii na kuhakikisha wananchi wanashiriki uchaguzi kwa hali ya utulivu.
“Kuanzia tarehe 2 tutakuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kampeni ya kuomba kura kwa wananchi. Tunawahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki na kushiriki katika uchaguzi huu wa amani,” alisema Monica.
Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi wa TANAPA, Iddy Kaluse, alisema Shirika la Hifadhi za Taifa limeamua kuunga mkono taasisi hiyo kwa sababu juhudi zake zinaendana na dhamira ya kuhamasisha utalii wa ndani.
“Tunatambua mchango mkubwa wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii wa ndani kupitia filamu ya Royal Tour. Tunawahimiza wananchi kujitokeze kwa wingi kutembelea hifadhi za taifa ili kujionea vivutio vyetu mbalimbali,” alisema Kaluse.
Taasisi ya Na Simama na Mama na TANAPA wameahidi kushirikiana kwa karibu katika kukuza uchumi wa taifa kupitia uwezeshaji wa wanawake na maendeleo ya utalii wa ndani, sambamba na kuhamasisha amani wakati wa uchaguzi.